Serikali imepiga marufuku Watumishi wa Umma waliohamia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa gharama za Serikali kuomba uhamisho wa kurejea jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro alipokuwa akifanya mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuhusiana na zoezi zima la uhamisho wa watumishi wa umma kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Dkt. Ndumbaro amesema kuwa, Ofisi yake imekuwa ikipokea barua mbili au tatu kwa siku za watumishi waliohamia Dodoma kuomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya wakati hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa ina vifaa vya kisasa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za matibabu kwa watumishi hao.
Dkt. Ndumbaro amefafanua kwamba, kabla ya watumishi kuhamia Dodoma, Serikali ilitoa maelekezo kwa waajiri kuwasilisha orodha ya watumishi wenye matatizo ya kimsingi ili wabaki kwenye vituo vya kazi vilivyopo Dar es Salaam wakiendelea kutekeleza majukumu yao.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, baadhi ya watumishi waliohamia Dodoma, wamegeuza uhamisho huo kuwa mradi wa kuwaingizia kipato kwani mara baada ya kuripoti Dodoma, ndani ya kipindi kifupi wanaomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam.
Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa, kutokana na suala hilo, Serikali imetoa Waraka wa Barua wenye Kumb. Na. CAC 228/257/01/A/53 wa tarehe 25 Septemba, 2018 kuhusu Uhamisho wa Watumishi Waliohamia Dodoma Kutekeleza Uamuzi wa Serikali Kuhamishia Makao Makuu ya Nchi Dodoma ambao unazuia mtumishi aliyehamishiwa Dodoma kwa gharama za Serikali kuomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam mpaka atimize miaka mitatu katika kituo cha Dodoma.
Watumishi wa Umma kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa.