Serikali imetoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho wawe wamepeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionesha kiasi cha tani wanazohitaji na lini watazichukua.
Hayo yamesemwa leo Novemba 9, 2018 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa tamko la serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho, ofisini kwake jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema kwenye msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu, walishuhudia kusuasua kwa minada ambapo serikali ilikutana na wanunuzi wa zao hilo katika kikao kilichoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli na kukubaliana kununua kwa bei isiyopungua shilingi 3000.
"Mwenye nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua kwani ofisi yangu ipo wazi saa 24 wana nafasi ya kuleta barua wakati wowote wakionesha nia yao na kiwango wanachohitaji, zaidi ya hapo serikali haitaruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena", amesema Waziri Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema kuwa baada ya kupita siku hizo serikali italazimika kufuta usajili kwa wafanyabiashara wote waliojisajili kununua zao hilo kwasababu walikubaliana kwenda kununua lakini hali inayoonekana sasa ni kama kumkomoa mkulima.
Akizungumza na wanunuzi wa korosho Oktoba 28, Rais Magufuli alimuagiza Waziri mkuu kusimamia manunuzi ya zao hilo kabla ya kulisimamia yeye maana anaweza kumuondoa endapo akishindwa.
"Waziri Mkuu hakikisha Bodi ya Korosho iliyopo chini yako unaisimamia, kama mtu hafanyikazi fukuza hata kama ni kila siku, ili unusuru maisha yako. Mimi sioni shida ya kumfukuza hata Waziri Mkuu kama mambo hayaendi", alisema Rais Magufuli.
Social Plugin