Uongozi wa klabu ya Stand United ya mkoani Shinyanga imetangaza kuwafungia wachezaji wake wawili kutokana na utovu wa nidhamu ikiwa ni pamoja na kutoroka kambini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mwenyekiti wa klabu hiyo ya Chama la Wana Dkt. Ellyson Maeja alisema wachezaji hao wamekuwa wakionyesha vitendo vya utovu wa nidhamu na wao kama viongozi wameona wachukue hatua kali za kinidhamu.
"Kwa mfano mchezaji Tarick Seif wakati timu imeenda kucheza michezo ya ligi Dar es Salaam viongozi walizungumza naye vizuri na akaahidi kujiunga na timu lakini ikawa ni kunyume hakujiunga na wenzake, kama uongozi tukamuandikia barua ya kumtaka kuripoti katika kituo chake cha kazi Shinyanga ili kama kuna mazungumzo tuzungumze na kutatua tatizo kama lipo lakini hakufanya hivyo, tumemfungia mwaka mmoja asipege mpira ndani na nje ya nchi",alieleza Dkt. Maeja.
Kuhusu mchezaji Sixtus Sabilo Maeja alisema mchezaji huyo aliondoka kambini bila kuaga wakati timu ikikabiliwa na mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Mahasimu wao Mwadui fc mchezo ambao Stand United walipoteza kwa kufungwa 1-0.
"Sixtus Sabilo aliondoka kambini bila kutoa taarifa kipindi ambacho tulikuwa tunakabiliwa na mchezo dhidi ya Mwadui fc ikapelekea tukapoteza mchezo ule ,lakini pia michezo mingine tukafanya vibaya mbele ya Coastal Union tukifungwa nyumbani na ule wa ugenini tukifungwa na Ruvu Shooting kiukweli amechangia sana sisi kupata matokeo mabaya" ,alisema Maeja.
Katika dirisha dogo la usajili ambalo limefunguliwa jana Novemba 15 mpaka Desemba 15 mwaka huu timu hiyo imepanga kufanya usajili wa kupata wachezaji katika maeneo ya ulinzi, Ushambuliaji pamoja na golikipa mmoja.
"Dirisha la usajili limefunguliwa nasi tutafanya usajili kwa kuongeza wachezaji katika maeneo ya ulinzi, ushambuliaji pamoja na golikipa mmoja, hatujafanya vizuri sana katika michezo yetu iliyopita ya ligi lakini tunaamini tutafanya usajili wenye tija utakaoisaidia timu" alisema.
Katika hatua nyingine Dkt. Ellyson Maeja alitolea ufafanuzi kuhusu sakata ambalo linaendelea kusambaa katika mitandao ya kijamii kuwa timu hiyo imefukuzwa katika Hostel walizokuwa wanaishi kutokana na kudaiwa kodi ya Pango, ambapo alisema kuwa ni kweli wanadai na hawajafukuzwa bali waliamua kuondoka baada ya mwenye nyumba kufunga milango.
" Hatujafukuzwa kilichotokea ni kwamba mwenye nyumba aliamua kufunga nyumba, nasi tukaamua kumuomba tutoe vitu vyetu ndani na vilitolewa na wanachama wetu na tukahamishia katika hostel nyingine, tunashukuru ilikuwa ni kipindi cha mapumziko kwa wachezaji jambo hili halijatuathiri sana maana wachezaji wakirudi basi watafikia katika Hostel nyingine ambazo tutakuwa tumeandaa...
Hivyo ifahamike kuwa hatukufukuzwa ni kweli anatudai pesa ya pango na kipindi hiki kipaumbele chetu ilikuwa kulipa mishahara ya wachezaji lakini naona hatukuelewana lugha ndio maana yakatokea haya lakini tutamlipa pesa yake pindi tukipata" alisema Maeja.
Timu ya Stand United inashika nafasi ya kumi na tatu katika msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara baada ya kushuka dimbani mara kumi na nne na kujikusanyia alama kumi na nne.
Na Isaac Edward Kisesa - Malunde1 blog
Social Plugin