Mchumi mwandamizi wa Mwanza, Kaswalala Elisha anashikiliwa na Takukuru mkoani hapa kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh300, 000 kutoka kwa mfanyabiashara.
Kwa kawaida Takukuru hutoa taarifa za watu wanaowashikilia kufanya makosa muda mfupi kabla ya kupelekwa mahakamani, lakini naibu mkuu wa Takukuru mkoa, Emmanuel Stenga alizungumzia suala la ofisa huyo wa Serikali bila ya kueleza atafikishwa mahakamani lini.
Stenga aliwaambia waandishi wa habari jijini Mwanza leo kuwa mtuhumiwa huyo alishirikiana na mtu mwingine kutenda kosa hilo Novemba 16, akiwa katika ofisi yake iliyopo katika majengo ya ofisi ya mkuu wa mkoa.
Alisema siku moja kabla ya kunaswa kwenye mtego uliowekwa na maofisa wa Takukuru, mtuhumiwa huyo pamoja na mwenzake ambaye bado anatafutwa walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu na mfanyabiashara huyo anayejihusisha na uuzaji wa vifaa vya maabara (jina linahifadhiwa) aliyefikisha taarifa Takukuru.
“Pamoja na mambo mengine, watuhumiwa walimtuhumu mfanyabiashara huyo kukwepa kodi na kuiuzia Serikali bidhaa feki na hivyo kumtaka kutoa Sh5 milioni ili asichukuliwe hatua za kisheria,” amesema Stenga.
Amesema kosa hilo ni kinyume cha kifungu cha 15 cha Sheria ya Takukuru ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.