Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umesema kuwa watanzania waache kumsemea Rais John Magufuli kuhusu milioni 50 alizotoa kwa ajili ya maandalizi ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Rais wa TFF, Wallace Karia amesema kuwa wameumia kwa kupoteza mchezo wao dhidi ya Lesotho ila wanaamini kwamba Stars itafuzu michuano hiyo kwa kuweza kushinda nyumbani na kuwataka wanaozungumzia masuala ya pesa za Rais Magufuli waache.
“Wanaozungumzia pesa alizotoa Rais waache kuzungumzia suala hilo kwa kuwa wanamsemea wakati yeye hajasema hivyo watulie, Rais anajua mpira na anafuatilia pia hivyo waache kufanya hivyo.
“Nina matumaini ya kuweza kufuzu kwa timu yetu hasa kutokana na uwezo wa kupata matokeo tukiwa nyumbani kama ambavyo tulifanya dhidi ya Cape Verde ndivyo tutakavyofanya dhidi ya Uganda,” alisema.
Rais Magufuli alitoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya maandalizi ya Stars kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Lesotho ambao wamepoteza kwa kufungwa bao 1-0 na aliwaagiza kuja na ushindi wakishindwa alisema watazitapika.