Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAMASHA LA TIGO FIESTA 2018 DAR LEO LAAHIRISHWA

Kamati ya maandalizi ya tamasha la Fiesta imesema tamasha hilo halitafanyika leo Jumamosi Novemba 24, 2018 kama ilivyopangwa, kwamba wananchi waliolipa viingilio watarejeshewa fedha zao.

Kamati hiyo imeeleza hayo  leo ikiwa ni saa chache baada ya manispaa ya Kinondoni kuzuia tamasha hilo kufanyika katika viwanja vya Leaders Club.
Kupitia barua inayosambaa katika mitandao ya kijamii manispaa hiyo imesema kuwa tamasha hilo limehamishiwa katika viwanja vya Tanganyika Peakers, badala ya Leaders Club.
Sebastian Maganga, mwenyekiti wa kamati ya Fiesta ametoa tamko la kusitishwa kwa tamasha hilo leo, akieleza kuwa waliolipa kiingilio watarejeshewa fedha zao.
“Kwa masikitiko makubwa tunatangaza kusitisha tukio la kilele cha msimu wa Tigo Fiesta 2018 lililopaswa kufanyika leo Novemba 24, 2018 katika viwanja vya Leaders Kinondoni Dar es Salaam. Sababu za kusitishwa kwa tamasha hili zipo nje ya uwezo wetu,” anaeleza Maganga.
“Tunaomba radhi kwa madhara yoyote yatakayojitokeza.  Tunatambua  kwamba wapenzi wa Tigo Fiesta Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam walishajiandaa vyema na tukio hili na zaidi ya yote wapo ambao walishanunua tiketi.”
Amesema walionunua tiketi kupitia Tigo Pesa, fedha zao zitarejeshwa moja kwa moja kwenye simu zao kupitia mtandao huo.
Amewataka walionunua kwenye vituo vya mauzo kufika kwenye vituo walivyonunulia wakiwa na tiketi zao kwa ajili ya kurudishiwa fedha.
Barua hiyo iliyoandikwa na ofisa utamaduni Manispaa hiyo jana Ijumaa Novemba 23, 2018 kwenda kwa waandaaji wa tamasha hilo, Clouds Media Group, ina kichwa cha habari kinachosema, kusitisha kibali cha kufanya Fiesta Leaders Club.
“Ofisi imepokea malalamiko ya wananchi na wagonjwa waliolazwa hospitalini kutokana na matangazo yaliyoambatana na muziki unaopigwa kwa sauti kubwa kutoka uwanja wa Leaders Club jambo ambalo linahatarisha afya za wagonjwa wakiwemo wa moyo,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
“Hivyo kwa barua hii nafuta kibali kilichotolewa Novemba 22, 2018 cha kufanya Fiesta uwanja wa Leaders na kuihamishia uwanja wa Tanganyika Peakers, Kawe.”
Katika ufafanuzi wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagulumjuli amesema, “Tumelizuia (tamasha) kufanyika hapo kwani uhai wa watu ni muhimu kuliko hicho kinachotaka kufanyika.
 “Jana tu walipokuwa wakitangaza hapo Leaders maeneo ya karibu kuna hospitali na watu wawili walizimia, sasa kwa njia hiyo hatuwezi kuruhusu furaha ya watu wengi ikawa majonzi kwa wengine.”
Amesema kwa hali ilivyo sasa hawawezi kuruhusu kufanyika kwa tamasha hilo viwanja vya Leaders hadi baadaye watakapojiridhisha ni salama kwa watu wengine.


Jana kuna barua ilisambaa mtandaoni....Kwa mujibu wa barua hiyo inayotajwa kutoka katika Ofisi ya Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Kinondoni imeeleza kuwa tamasha hilo lihamishiwe viwanja vya Tanganyika Peakers - Kawe.


Sababu za kusitishwa kwa kibali ni kutokana na malalamiko ya wananchi na wagonjwa waliolazwa hospitalini wanaodai muziki mkubwa na matangazo vinawapa usumbufu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com