Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe asomewa mashtaka matatu ya uchochezi, yenye nia ya kuleta chuki kwa Watanzania dhidi ya Jeshi la Polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo ,Zitto amekana kwa kusema sio kweli na muda huu yupo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akisubiri uamuzi wa dhamana.
Zitto Kabwe amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam leo Novemba 2,2018 baada ya kushikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Oktoba 31, 2018.
Zitto anatuhumiwa kutoa taarifa za uongo kuhusu mauaji ya baadhi ya askari polisi na wananchi katika kijiji cha Mpeta, wilayani Uvinza mkoa wa Kigoma.
Zitto, mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa nchini, mara baada ya kukamatwa alipelekwa kwenye Kituo cha polisi cha Oysterbay, kabla ya kuhamishiwa polisi kati na baadaye kulazwa kwenye kituo cha polisi Mburahati.
Kabla ya kukamatwa na Polisi, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno, alimtaka Zitto kuwasilisha alichokiita, “vielelezo vya madai yake,” kuwa watu zaidi ya 100 wameuwa katika eneo la Uvinza.