WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema Jeshi la Polisi lipo imara kupambana na uhalifu wa aina yoyote utakaojitokeza nchini hivyo wahalifu wasithubutu kulichezea, wala ‘kulibipu’.
Lugola pia amewataka wananchi kuendelea kuwapa taarifa za uhalifu Polisi ili ziweze kufanyiwa kazi haraka kwa kuwa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli si ya kuchezewa na imejipanga kikamilifu kwa kuwalinda wananchi wake.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Ragati, Kata ya Kasuguti, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, Lugola alisema Jeshi la Polisi lipo imara na litaendelea kuwalinda wananchi pamoja na mali zao, ila Polisi ili waweze kufanya kazi zao kwa umakini zaidi, wananchi wanapaswa kuwasaidia katika kufichua uhalifu katika maeneo yao wanayoishi.
Lugola aliyazungumza hayo baada ya wananchi wa Kijiji hicho kumlalamikia kuwa kuna kundi la vijana ambalo linaongozwa mwananchi mmoja kijijini hapo wanahatarisha amani na kuwafanya kuishi kwa wasiwasi na kushindwa kufanya shughuli zao za maendeleo.
“Polisi wapo kwa ajili yenu hivyo kuweni huru muda wowote kutoa taarifa za kiuhalifu katika maeneo yenu, hivyo kutokana na viashiria hivyo vya uvunjifu wa amani katika Kata hii namuagiza mkuu wa polisi wilaya (OCD) kuwasaka, kuwakamata wale wote ambao wanahatarisha amani katika Kata hii ya Kasuguti,” alisema Lugola. Lugola aliongeza kuwa, yeye ni Mbunge wa Jimbo hilo na pia ni Waziri ambaye anasimamia usalama wa wananchi na mali zao, hivyo hatakubali wananchi waishi kwa wasiwasi katika maeneo yao na nchi kwa ujumla, na pia Serikali ya Magufuli haichezewi, haijaribiwi na wala haibipiwi na mtu yeyote.
Amesema licha ya polisi usiku na mchana wanalinda wananchi na mali zao lakini pia wananchi ni wadau wakubwa kwasababu wana mengi wanayaona mitaani kwao hivyo kwa baadhi ya wale wenye tabia ya kuficha matukio ya uhalifu ni hatari kwa usalama wao. Aidha, Lugola aliwataka wananchi wa Kata hiyo waendelee kufanya shughuli za kimaendeleo katika vijiji vyao na pia waanze maandalizi ya kilimo, naye atahakikisha anatoa misaada mbalimbali ikiwemo mbegu ili wananchi hao waweze kupata mazao yaliyo bora kwa hapo baadaye.
Lugola pia alijibu maswali mbalimbali ya wananchi hao, yakiwemo kuhusu maendeleo ya Jimbo lao na pia kuhusu Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuhusu kuwapa vitambulisho. Hata hivyo, kwa upande wa wananchi kupata vitambulisho vya taifa, Lugola aliendelea kusisitiza kuwa, Vitambulisho hivyo vitatolewa kwa watanzania wenye sifa na haki yao kupata lakini ili waweze kupata vitambulisho hivyo lazima wapitie katika mchujo ili kuepusha kutoa kwa wasio raia.
Amesema mchujo huo unaofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) upo makini ili kuhakikisha hakuna makosa yatakayofanywa wakati wa utoaji wa vitambulisho, hivyo wananchi wawe na uvumilivu wakati mchujo huo ukiendelea. Lugola anaendelea na ziara jimboni kwake akisikiliza kero za wananchi pamoja na kuhamasisha kilimo cha mazao ya pamba, mahindi, mpunga, viazi na mengineyo ambayo wakazi wa jimbo lake wanalima mazao hayo kwa wingi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola (kulia), akimsindikiza kumpeleka ndani ya gari Mkazi wa Kitongoji cha Songambele, Kata ya Kasuguti, Jimbo la Mwibara mwenye umri wa miaka 100, Mzee Mtatiro Silla, mara baada ya Waziri huyo kumaliza mkutano wake wa hadhara akizungumza na wananchi wa Kata hiyo, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo.
Lugola aliwataka wananchi jimboni kwake watoe polisi taarifa za uhalifu nchini na pia Serikali ya Awamu ya tano ipo imara haichezewi na mtu yeyote. Pia Lugola aliwataka wananchi jimboni kwake waanze maandalizi ya kilimo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Social Plugin