Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AAGIZA WAKULIMA WA KOROSHO WALIPWE FEDHA ZAO KWA HARAKA

Na Bakari Chijumba, Mtwara
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya ziara ya siku moja wilayani Nachingwea Mkoani Lindi jana Tarehe 17 Nov 2018 ambapo ameusihi Uongozi wa Mkoa na wilaya, uendeleee kusimamia kikamilifu na kwa haraka zoezi la uhakiki na malipo kwa wakulima wa korosho msimu wa 2018/19.


Waziri Mkuu aliwasili wilayani humo mapema jana na kupokelewa Katika uwanja wa ndege wa Nachingwea na Viongozi wa Mkoa wakiongozwa na Rc Godfrey Zambi na Wale wa Wilaya wakiongozwa na Dc Rukia Muwango, pamoja na Viongozi wengine na kisha kufanya ziara katika tarafa ya kilimarondo akipitia pia vijiji kadhaa kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wanachi na kukagua miradi mbalimbali.


Taarifa iliyotolewa na Mbunge wa Nachingwea Hassani Masala kuhusu mrejesho wa Ziara hiyo inasema, akiwa wilayani humo, Waziri mkuu pia ametimiza ahadi yake kwa wananchi wa Mpiruka kwa kuwapatia saruji kwa ajili ya ujenzi wa shule Mpiruka A, na Kiasi cha tani mbili na nusu kimekabidhiwa kwa uongozi wa kijiji.


Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewahikikishia Wakazi wa Nachingwea kuwa Ujenzi wa uwanja wa ndege Nachingwea utaanza muda sio mrefu Kutoka sasa na Mkandarasi ashapatikana na kazi inapaswa kuanza mara moja.


"Kukamilika kwa Uwanja huu wa ndege kutarahisisha huduma za ndege wilayani Nachingwea kuboreshwa hivyo kusaidia wilaya zote za jirani" amesema waziri Mkuu


Taarifa hiyo ya Mbunge Masala inaendelea kusema kuwa, Waziri Mkuu amepokea salam za Pongezi kutoka kwa wazee wa Nachingwea kwenda kwa Mh Rais kwa kujali na kupigania maslahi wakulima na wanyonge huku pia Waziri Majaliwa akiagiza kukamilishwa kwa Zahanati ya kijiji cha Namatula kwa kutoa miezi isiyozidi mitatu kwa Ofisi ya Mkurugenzi Iwe imekamilisha zahanati hiyo iliyoanza kwa nguvu za wananchi, ofisi ya mbunge na Halmashauri yenyewe.


Katika hatua nyingine Waziri mkuu ameagiza idara ya MANAWASA kupeleka maji vijiji vya Namatula A & B kwa haraka sana kutoka kwenye chanzo cha maji ya Mbwinji na amewahakikishia wananchi wa Nachingwea vijiji vyote vya wilaya ya Nachingwea kupatiwa umeme vijijini kwa awamu mbili na kazi imeshaanza tayari.


"Mhandisi wa maji wilaya peleka haraka barua ya kuomba pesa wizara ya maji na nakala niipate ili Kulipa mkandarasi anayesambaza maji kwenye kijiji cha Mtua ili kuharakisha kupatikana kwa huduma ya maji ifikapo mwezi wa kwanza na nataka wapelekwe watumishi wa afya katika zahanati ya Mtua na kituo cha Afya Kilimarondo mara moja' Ameagiza Waziri Mkuu


Waziri Mkuu ameagiza pia kuanza kazi ya kuchimba visima viwili ifikapo jumatatu tarehe 19 katika kijiji cha Mbondo na amekagua ujenzi wa kituo cha Afya Kilimarondo na kutoa maagizo ya kupatikana pesa toka Halmashauri ili kukamilisha ujenzi wa kituo hicho ambao umesuasua kukamilika kutokana na kuishiwa pesa.


"Kituo hiki kitapatiwa kiasi cha Tsh. milioni 230 pindi ujenzi utakapokamilika kwa ajili ya kununua vifaa tiba na naiagiza ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuunda timu itakayopitia hesabu za fedha za ujenzi wa kituo hiki na sababu zinazopelekea kutoanza ukarabati kwa hospital ya wilaya Nachingwea pamoja na kupatiwa pesa toka mwezi wa saba mwaka huu" amesema waziri Mkuu


Mh Waziri Mkuu pia, amepokea ombi la wananchi wa Kilimarondo juu ya kugawa jimbo na kufunguliwa kwa barabara Inayounganisha Tunduru na Nachingwea kupitia Lumesule,Ngapa,Namatunu na amepokea ombi la mbunge Massala la kupatiwa gari ya wagonjwa kwa ajili ya kituo cha Afya Kilimarondo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora.


Waziri Mkuu Majaliwa amewahakikishia wananchi wa Nachingwea juu ya kupatikana kwa mkandarasi atakayeanza kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Masasi, Nachingwea ,Ruangwa hadi Nanganga na kusema kazi ya Upembuzi yakinifu kwa barabara ya kutoka Nachingwea kwenda Liwale imeshaanza.


Mh Waziri mkuu pia ametawazwa kuwa kiongozi wa wangindo kwa kuvishwa na kukabidhiwa zana mbalimbali kama shukrani kwa heshima kubwa aliyowaonyesha watu wa tarafa ya kilimarondo.


Kwa upande wake Mbunge Massala ametoa Shukrani kwa Raisi Magufuli na serikali yake yote chini ya usimamizi wa Mh waziri Mkuu kwa kuwajali wananchi na kupigania Maendeleo yao kwa kadiri ya ahadi zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com