WAZIRI MKUU AMTUMBUA MHASIBU WA HALMASHAURI

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amsimamishe kazi aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Mbogwe, Adam Nyoni kwa tuhuma za ubadhilifu wa sh. milioni 19.4 za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Kadhalika Waziri Mkuu ameagiza Mhasibu huyo ambaye awali alikuwa wa Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe na sasa amehamishiwa halmashauri ya wilaya ya Nyag’hwale arudishwe Mbogwe na asimamishwe kazi huku shauri lake likifikishwa katika vyombo vya sheria.


Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Novemba 29, 2018) alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Masumbwe wilayani Mbogwe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Geita.


Waziri Mkuu aliwataka watumishi wote wa umma wawajibike katika kufanya kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu na haitosita kuwachukulia hatua.


“Serikali hii haitamuhamisha wala kumuundia tume mtumishi atakayetafuna fedha za umma, ukiharibu tunamalizana hapo hapo. Naagiza mtumishi huyo aliyehamishiwa Nyang’hwale arudishwe hapa kwa kuwa kabla ya kuhamishwa kulikuwa na upotevu wa sh. milioni 19.4.”


Alisema watumishi wa umma wanapaswa wawatumikie wananchi bila ya ubaguzi wowote pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea. “Lazima mtambue kwamba msimamo wa Serikali ni kuwahudumia wananchi bila ya ubaguzi wa kidini, kiitikadi na kipato.”


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi kwenda katika ngoma za usiku za chagulaga na kuwachukulia hatua wanaume wote wanaowachagua wanafunzi wa kike kwa kuwa wanawaharibia maisha.


Alisema lazima wananchi washirikiane na Serikali katika kuwalinda wanafunzi wa kike ili wasipate ujauzito na kukatisha masomo yao kwa sababu kitendo cha kupata ujauzito kinawafanya wakatishe masomo yao jambo ambalo linakwamisha kufikia lengo lao kielimu.


Kadhalika, Waziri Mkuu alipiga marufuku kwa wanafunzi hao wa kike kuhudhuria kwenye ngoma hiyo ya usiku na badala yake watumie muda mwingi kujishughulisha na masuala ya masomo ili waweze kutimiza ndoto zao. “Wanafunzi wa kike msikubali kushawishika."


Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi wa wilayani Mbogwe kuhakikisha watoto wenye umri wa kuanzia miaka minne kuwapeleka shule ili waanze darasa la awali na kwamba hawatakiwi kutoa mchango kwa kuwa Elimumsingi inatolewa bure nchini.


Hata hivyo, Waziri Mkuu aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwekwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali la kujenga Zahanati katika kila kijiji kwa kuwa wilaya hiyo inaendelea na shughuli za ujenzi wa Zahanati katika vijiji 82 kati ya vijiji 86.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post