Mwigizaji na mlimbwende wa Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shitaka la kuchapisha video yake ya ngono kupitia kurasa yake ya Instagram, mashitakiwa amekana makosa na kuachiwa kwa dhamana,leo Alhamisi Novemba Mosi, 2018.
Msanii huyo wa Filamu nchini, amesomewa kosa hilo na Wakili wa Serikali Mwanaamina Kombakono mbele ya Hakimu Mkazi, Maila Kasonde, amedai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja la kuchapisha video ya ngono kinyume na sheria.
Wema anadaiwa kutenda kosa hilo, Oktoba 15, 2018 katika sehemu tofauti tofauti ambapo alichapisha kupitia mtandao wake wa Instagram video yake ya picha za kingono kitu ambacho hakiruhusiwi, msanii huyo amekana kufanya kosa hilo.
Baada ya kukana wakili wa utetezi, Semwanza Rubeni alimuombea dhamana mteja wake.
Hata hivyo, Wakili wa serikali Kombakono amedai kuwa licha ya dhamana ni haki ya Kikatiba anaiomba mahakama imuwekee masharti magumu kwa sababu Wema anafuatiliwa na idadi kubwa ya watu kupitia mtandao wake wa Instagram ikiwemo watoto.
Katika uamuzi wake, Hakimu Kasonde amesema anatoa masharti ya dhamana ambapo Wema anatakiwa asaini Bondi ya Sh. 10 milioni na awe na mdhamini mmoja atakayesaini kiasi hicho.
Pia amesema anatakiwa asiweke picha yoyote yenye maudhui ya ‘Ngono’ kwenye mtandao wake wa Instagram wala maneno yenye uelekeo ama viashiria vya kingono.
Wema ameachiwa kwa dhamana, kesi imeahirishwa hadi Novemba 11, 2018.
Chanzo- Mwanahalisi Online
Social Plugin