Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Habari wa TACAIDS Bw. Jumanne Issango akifunga Ariel Camp 2018 kwa niaba ya Mkurugenzi wa TACAIDS.
Kambi ya watoto na vijana inayosimamiwa na Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) maarufu kama Ariel Camp 2018’ iliyoshirikisha washiriki 50 kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu imefungwa leo Ijumaa Disemba 14,2018 jijini Dar es salaam.
Akifunga kambi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS), Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Habari wa Tume hiyo Bw. Jumanne Issango aliipongeza AGPAHI kwa kuanzisha kambi hizo zinazolenga kuwapa watoto na vijana msaada wa kisaikolojia utakaowawezesha kukabialiana na changamoto zinazowakabili.
“Naishukuru AGPAHI kwa kutoa msaada huu wa kisaikolojia kwa watoto na vijana kwani huduma hiyo ni muhimu sana kwa afya na ustawi wao hasa ikizingatiwa kuwa changamoto hizo zinawaathiri kimwili, kiafya, kijamii na kisaikolojia,” alisema Bw. Issango.
Aidha aliitaka jamii kubadilika na kuacha vitendo vya kunyanyapaa wanaoishi na maambukizi ya VVU huku akiwahamasisha watoto na vijana hao kutumia kwa usahihi dawa za kufubaza makali ya VVU ili kuimarisha afya zao.
“Ili kuishi maisha bora na kukamilisha ndoto zenu za baadaye nawakumbusha kuwa ARV ndiyo mpango mzima, Watu wasiotumia vizuri dawa hizi afya zao zimekuwa zikitetereka na kushambuliwa na magonjwa nyemelezi na hata kufa. Kamwe msiache kutumia dawa kwa sababu yoyote ile,” alisisitiza.
Pia aliiomba AGPAHI kwa kushirikiana na watoa huduma na wadau mbalimbali kuelimisha wananchi kuhusu VVU na maambukizi yake kwani imedhihirika kuwa bado jamii haina elimu ya kutosha kuhusu VVU na UKIMWI. "Kudhihirika huku kunatokana na unyanyapaa unaoendelea katika jamii."
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taarifa za Kimkakati wa AGPAHI, Dk. Boniface Idindili, aliziomba halmashauri za wilaya kutenga bajeti kwa ajili ya kuanzisha klabu za vijana na watoto wanaoishi na VVU na kupata huduma za tiba na matunzo katika vituo vya afya ili wengi zaidi waweze kupata msaada wa kisaikolojia.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Idindili alisema, “Tunaiomba serikali iweke madawati maalumu mashuleni na kwenye vyuo kwa ajili ya kusaidia watoto na vijana wanaoishi na VVU, Vijana wengi hulazimika kukabiliana na changamoto zao kimya kimya kwa kukosa msaada na wakati mwingine hushindwa kuzimudu.”
Pia alishauri vyuo vya ufundi stadi vya VETA kutoa upendeleo maalum kwa vijana wanaoishi na VVU kujiunga navyo ili kuwawezesha kujitegemea na kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Nao washiriki wa Kambi ya Ariel walisema kuwa kipindi chote wakiwa kambini wamefundishwa mambo mengi yaliyowasaidia kuwajenga kiakili na kimwili.
Katika risala yao kwa mgeni rasmi, walitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na ujasiriamali, matumizi sahihi ya dawa, ukatili wa kijinsia na unyanyapaa.
Mbali na kubadilishana mawazo na kupata marafiki wapya, washiriki wamecheza michezo mbalimbali na kutembelea Mji wa Kihistoria wa Bagamoyo ili kujifunza kiundani historia ya Tanzania.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Habari wa TACAIDS Bw. Jumanne Issango akizungumza katika ukumbi wa Serene Beach Resort wakati akifunga Ariel Camp 2018 kwa niaba ya Mkurugenzi wa TACAIDS. Kushoto ni Mkurugenzi wa Taarifa za Kimkakati wa AGPAHI, Dk. Boniface Idindili,kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za mama na mtoto AGPAHI, Dk. Akwila Temu.
Waliokaa ni washindi wa shindano la Mr & Miss AGPAHI Ariel Camp wakiwa katika picha ya pamoja na jaji Lugano Maclean (wa kwanza kulia) na kiongozi wa washiriki wa shindano la Urembo 'Mr & Miss Ariel Camp' Agnes William ( wa kwanza kushoto) na washiriki wa shindano hilo.
Keki ya upendo kwa ajili ya washiriki wa Ariel Camp 2018.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Habari wa TACAIDS Bw. Jumanne Issango akimlisha keki mshiriki wa Ariel Camp 2018.
Miss Ariel Camp 2018 akimlisha keki Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Habari wa TACAIDS Bw. Jumanne Issango.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Habari wa TACAIDS Bw. Jumanne Issango akikabidhi zawadi ya begi kwa mshiriki wa Ariel Camp 2018. Mabegi hayo ya shule yamekabidhiwa kwa washiriki wote 50 wa Ariel Camp 2018.
Kijana akifurahia baada ya kupewa zawadi ya begi la shule.
Watoto wakiwa wamekaa na mabegi yao.
Washindi wa shindano la Mr & Miss Ariel Camp 2018 wakifuata zawadi kwa mgeni rasmi.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Habari wa TACAIDS Bw. Jumanne Issango akikabidhi zawadi ya saa za ukutani kwa washindi wa shindano la Mr & Miss Ariel Camp 2018.
Vijana na watoto wakiwa na walezi wao waliojichora rangi usoni.
Latifa Abdallah kutoka Taasisi ya Babawatoto akitoa burudani ya kuzungusha meza kwa miguu.
Kijana wa Babawatoto Debora Dickson akitoa burudani ya sarakasi.
Mtoto akielezea kuhusu mchoro aliochora kwa Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Habari wa TACAIDS Bw. Jumanne Issango na Mkurugenzi wa Taarifa za Kimkakati wa AGPAHI, Dk. Boniface Idindili.
Picha ya pamoja mgeni rasmi na washiriki wa Ariel Camp 2018.
Picha ya pamoja Mmiliki wa Hoteli ya Serene ambapo ndipo kambi ya vijana na watoto imefanyika, Dk. Moses Mkonye (wa pili kulia) na watoto wawili aliojitolea kuwasomesha na Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Habari wa TACAIDS Bw. Jumanne Issango (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Huduma za mama na mtoto AGPAHI, Dk. Akwila Temu (wa kwanza kushoto) na Mkurugenzi wa Taarifa za Kimkakati wa AGPAHI, Dk. Boniface Idindili (wa kwanza kulia).
Vijana wakipiga picha ya kumbukumbu baada ya Ariel Camp 2018 kufungwa.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Vijana wakipiga picha ya kumbukumbu baada ya Ariel Camp 2018 kufungwa.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Social Plugin