Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imepokea jumla ya maombi 594,300 kutoka kwa waombaji wa nafasi za kazi katika Utumishi wa Umma zilizotangazwa katika Wizara, Idara, Wakala, Sekretarieti za Mikoa, Manispaa, Halmashauri na Taasisi za Umma kuanzia Mwezi Novemba 2015 hadi Desemba 2018.
Akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka mitatu ya Taasisi hiyo (2015-2018) jana Desemba 17, 2018 Jijini Dar es Salaam, Katibu wa Sektretarieti ya Ajira, Xavier Daudi alisema tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali imetangaza nafasi zilizo wazi 6,554 ambapo jumla ya waombaji 140,000 waliitwa katika usaili.
Daudi aliongeza kuwa hadi kufikia Desemba 15 mwaka huu jumla ya nafasi wazi za kazi 6,099 zilikwishajazwa, ambazo nafasi 455 zilizotangazwa kati ya mwezi Novemba na Desemba mwaka huu mchakato wake unaendelea na kukamilika hivi karibuni.
Aidha Xavier alisema mbali mchakato huo unaoendeshwa na Ofisi yake, pia wapo watumishi walioajiriwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kada za Afya na Walimu, ambapo katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya watumishi wa kada za afya 24,728 wameajiriwa wakati kwa upande wa kada ya ualimu jumla ya walimu 40,086 waliajiriwa Serikalini.
“Idadi hii inaweza kuongezeka katika mwaka huu wa fedha 2018/19 kwa watumishi watakaoajiriwa kwa kada za walimu, afya pamoja na watumishi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama ambao utaratibu wake wa ajira unataratibiwa na mamlaka husika” alisema Xavier.
Akizungumzia kuhusu udhibiti wa waombaji wasio na sifa ikiwemo wenye vyeti feki vya kughushi, Xavier alisema Ofisi yake imeendelea kukagua nyaraka za waombaji mbalimbali ikiwemno vyeti vyao ili kuhakikisha kuwa wanaoajiriwa Serikalini ni wale wenye sifa na vyeti vinavyostahili kwa mujibu wa sheria.
Akifafanua zaidi, Xavier aliongeza kuwa katika yam waka 2015-2018 jumla ya nyaraka za vyeti vya waombaji kazi 18,817 viliwasilishwa kwenye mamlaka zinazohusika na utoaji wav yeti hivyo kwa ajili ya uhakiki, ambapo jumla ya vyeti halali vilikuwa 18,112 na vyeti 706 vilibainika kuwa ni vyeti vya kughushi.
Kuhusu uimarishaji wa mfumo wa matumizi ya Tehama katika mchakato wa ajira, Xavier alisema Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza katika matumiZi ya TEHAMA ili kurahisisha utoaji hudumazake kwa kupitia TEHAMA na kuanzisha mfumo wa kielectroniki kwa watumiaji wa maombi ya kazi ujulikanao kama ‘Rectruitment Portal’ unaopatikana katika anuani ya portal.ajira.go.tz.
“Mfumo huu ulianza kutumika mwaka 2014/15 hadi kufikia tarehe 15 Desemba mwaka huu zaidi ya watu 300,500 wamejiandikisha na maombi ya kazi yaliyowasilishwa kupitia mfumo huu ni zaidi ya 594,200” alisema Xavier.
Kwa mujibu wa Xavier alisema tangu kuanzishwa kwake, Mfumo huo umekuwa na mafanikio makubwa kwani umesaidia kupunguza mchakato wa ajira kutoka siku 90 hadi kufikia siku 52 na hivyo kupunguza malalamiko ya waombaji kazi kuhusu upotevu wa barua zao za maombi ya kazi pamoja na kupunguza ufinyu wa nafasi ya kutunza nyaraka za maombi ya kazi.
Social Plugin