Ameandika Dotto Bulendu kwenye ukurasa wake wa Facebook
Tatizo la ajira kwa vijana nchini Tanzania ni kubwa kuliko tatizo la kikokoteo cha mafao ya kustaafu.
Kama tulivyopiga kelele kuitaka Serikali itazame upya uamuzi wake wa kuwalipa wastaafu asilimia 25 ya mafao yao ya kustaafu na kilichobaki walipwe kidogo kidogo,kelele hizo hizo zinatakiwa kupigwa ili tupate ufumbuzi wa tatizo la ajira nchini maana tunajitengeneza bomu wenyewe.
Ikiwa kati ya Mwaka 2015 mpaka Disemba 18.2018 Jumla ya vijana Laki tano ,tisini na nne elfu na mia tatu(594,300)waliomba kazi serikalini na waliopata kazi walikuwa ni elfu sita na mia tano hamsini na nne(6,554) ukiwa ni wastani wa watu mia moja(100) wanaoomba kazi serikalini ni mmoja tu ndiye mwenye uhakika wa kupata kazi,tunahitaji kupiga kelele,kushauri,kuonya juu ya athari za kuwa na kundi kubwa la vijana wanaosaka kazi.
Rafiki yangu mmoja aliandika mtandaoni kuwa vijana wengi ni "Book Smart" huku wakikosa ujuzi wa namna ya kukabili changamoto za mtaani (Street smart)ndiyo maana tuna kundi kubwa la vijana waliokata tamaa na maisha huku wakiwa na shahada zao mkononi.
Kama ni hivyo lazima tuje na mpango wa haraka utakaobadili elimu yetu ili vijana hao wenye shahada zinazovutia ila wanahangaika mtaani wanapokuwa vyuoni mpaka vyuo vikuu wapate vyote, yaani wawe "Book smart" na "street smart",wazijue fursa zilizopo mtaani na namna ya kuzitumia ili tujinasue na hatari ya kuwa na kundi kubwa la vijana wasio na kazi.
Kama ndani ya miaka mitatu vijana zaidi ya laki tano na nusu walipambana kusaka kazi serikali na wakapata watu elfu sita na mia tano, hii maana yake nini?kufikia mwaka 2020 tunaweza kubwa na kundi kubwa linalopindukia vijana milioni moja wenye sifa za kitaaluma na wapo nyumbani hawana cha kufanya,maana vyeti vyao vyenye GPA haviwapi kazi wala hawawezi vitukia kupata mkopo benki wala serikalini.
Hivi karibuni,shirika la afya duniani lilipata kusema vijana milioni 3.7 wanaugua ugonjwa wa Sonona(Depression),kutokana na changamoto za maisha wanazokutana nazo ikiwemo ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha,achilia mbali sababu za kimahusiano na usaliti kwenye ndoa zao.
Vijana nchini Tanzania sasa wanakutana na fursa chache za ajira huku wale waliomo makazini wakikumbana na changamoto za kulipwa kidogo,kukopwa mishahara yao huku wakifanyishwa kazi kwa muda mrefu na katika mazingira magumu.
Vijana wengi walio makazini wanakilio cha kukaa kazini muda mrefu bila kupandishiwa malipo yao huku ukali wa maisha ukipanda kila kukicha,lakini hili ni kundi dogo,kundi kubwa lipo mtaani.
Nilipokuwa namsikiliza Rais John Magufuli wakati akizungumzia sakata la kikokoteo ,alisema mpaka mwaka 2023 kutakuwa na wastaafu takribani elfu 58 watakaotakiwa lipwa mafao,hawa kilio chao kimesikika.
Tujiulize kwa pamoja,kama kati ya mwaka 2015 mpaka Disemba 2018 vijana zaidi ya laki tano waliomba kazi serikalini na laki tano na zaidi wakakosa,je mpaka kufikia mwaka 2023 tutakuwa na kundi la vijana wangapi wanaopambania kazi serikalini?
Sasa hivi sekta binafsi imepunguza kasi ya kuajiri ,inachokifanya sasa ni kupunguza wafanyakazi wake na kimbilio lake ni serikali ambayo watu ambao imewaajiri hawafiki hata milioni moja!
Tunawasaidiaje vijana wetu wenye changamoto ya kuwa "Book smart"?je tuwalaumu tu kuwa wamesoma na hawajui maisha ya mtaani?na je ni kweli shuleni,vyuoni mpaka vyuo vikuu vijana wetu hawafundishwi namna ya kuyaishi maisha ya mtaani na changamoto zao?kama ndiyo nani alaumiwe?je ni wao ndiyo waliotengeneza mtaala ambao mwisho wa siku unawaacha wakiwa "Book smart" wasiojua maisha ya mtaani?
Tunawasaidiaje vijana wetu?
Juzi nilikuwa nasafiri kati ya Mwanza na Shinyanga nikapita eneo linaitwa Mabuki nikaambiwa wakati wa Nyerere kulikuwa na mashamba makubwa ya mazao na mifugo leo pamebaki hamna kitu,tukifufua hapo tutaajiri vijana wangapi?
Nilipofika Shinyanga nikaona kiwanda cha Nyama kimefungwa,nikauliza mbona wasukuma wanafuga na watu wanakula nyama kwa nini hakifanyi kazi?sikupata majibu na ninaambiwa kiwanda hiki kilijengwa mwaka 1974 na Mwalimu Nyerete,tukifufua hiki tutaajiri vijana wangapi?
Hapa Mwanza kila nikienda Airport napita kiwanda cha Ngozi Ilemela,huwa nakumbuka siku moja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015,Rais Magufuli akiwa mgombea alisema akishinda atahakikisha kiwanda hicho kinafufuka na akatoa siku saba kianze kazi.
Kiwanda hicho kilijengwa na Serikali ya Nyerere,lakini jana nimepita hapo sioni kinachoendelea,najiuliza kwani wasukuma hawafugi tena?kwani watanzania hawavai viatu vya ngozi?tukifufua hiki kiwanda tutaajiri vijana wangapi?
Kila napoenda Nyakato hupita kiwanda cha nguo ya Mwatex,nchi kilijengwa na Serikali ya Nyerere lakini sasa sioni kinachoendelea,najiuliza dada na mama zetu hawavai tena kanga?wasukuma hawalimi tena pamba?tukifufua hiki kiwanda tutatengeneza ajira ngapi?
Ni kama nilipokwenda Tabora wiki mbili zimepita nikaambiwa kile kiwanda cha nyuzi kilichokuwa kinaajiri kundi kubwa la vijana pale Tabora nacho ni kama kishaenda halijojo kitambo,nikajiuliza hivi watanzania hawashoni? siku hizi?nguo zao hazichaniki?nikaambiwa nyuzi siku hizi zinatoka China,nikajiuliza hivi tukifufua hiki tutaajiri vijana wangapi?
Bahati mbaya sana,fikra za viongozi wetu ni kuwa wanadhani serikali itajenga viwanja,itarejesha,italima na kuendesha mashamba makubwa ,Itafuga mifugo,itavua yenyewe.
Tusipoamua kuotekeleza Sera ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi,sera ya wazawa ili kuhakikisha tunatengeneza matajiri wakubwa wazawa wakashikilia njia kuu za uchumi kwa ubia na serikali huku tukiwa wakali kwenye Rushwa hatutatoka abadani.
Tunawalaumu vijana na kuwataka wajiajiri,je tumewapa mitaji?maana siku hizi utawasikia watu wanasema wewe ukiwa na wazo tu unatoka,unabaki na maswali hivi hawa vijana laki tano wote hawana mawazo ya kujiajiri kweli?
Ukimsikiliza anayesema hivyo yeye alianza na mtaji wa zaidi ya milioni kumi,tena yupo kazini,kachukua mkopo kwa dhamana ya kazi yake,hawa vijana masikini hawa tunawasaidiaje na vyeti vyao vya chuo kikuu?
Hebu serikali ijaribu kuwaambia hawa vijana kuwa Cheti chako cha stashahada,shahada,shahada ya uzamili ama uzamivu kinaweza kuwa dhamana ya kuchukuliwa mkopo kwa Riba ndogo na tuwe na mpango kabambe wa kuwafanya vijana wetu wazijue fursa zilizopo ndani na nje ya nchi kutoka sekta ya kilimo,uvuvina ufugaji tuone kama utawaona wa akimbizana Wizara ya Utumishi kuomba kazi.
Vijana wetu wanahitaji zaidi ya hiki wanachopata vyuoni,wanahitaji "Skills" zaidi na binafsi wengi naowafahamu mimi wana "Skills" za kutosha katila maeneo waliyoyasomea lakini wanakosa mtaji ili wajiajiri wenyewe.
Tunaweza jidai hatuoni,hatusikii sauti zao,lakini ukweli ni kwamba tatizo la ajira kwa vijana tukilibeza na kubaki kupigana vijembe,tunatengeneza bomu kubwa na kuongeza idadi ya vijana wanaougua Sonona.
Wasalaaam
Social Plugin