Klabu ya soka ya Coastal Union kutoka jijini Tanga, imekanusha vikali taarifa zinazoeleza kuwa mchezaji wao, Ali Saleh Kiba maarufa kama Alikiba amevunja mkataba kama mchezaji na kuwa kiongozi wa timu hiyo.
Coastal imesema taarifa hizo zilizoanza kusambaa mitandaoni jana Desemba 10, 2018, sio za kweli na zinatakiwa kupuuzwa kwani zinalenga kuichonganisha timu na wadhamini wake akiwemo yeye mwenyewe Alikiba kupitia kinywaji chake cha MoFaya.
''Habari hizo ni za uongo na zina lengo la kutuvuruga na kuudanganya umma, hakuna hata neno moja lenye ukweli na Coastal Union ina laani kitendo cha Mwandishi kuandika habari isiyo na chembe ya ukweli'', Umeeleza uongozi wa Coastal.
Aidha klabu hiyo imetoa ufafanuzi kuwa Ali Saleh Kiba sio kiongozi wa timu kama ilivyodaiwa badala yake ni mchezaji wa Coastal union kama wachezaji wengine japo ni mdhamini pia kupitia kinywaji chake.
Coastal kwa sasa inashika nafasi ya 6 ikiwa na alama 23 kwenye msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara baada ya michezo 16. Alikiba aliichezea Coastal Union kwa mara ya kwanza kwenye ligi kuu, Jumapili Desemba 9, 2018 ilipotoka sare ya 1-1 na Mbeya City.
Social Plugin