Baadhi ya mashine (Microscopes) zilizotolewa na taasisi ya APHFTA ili kusaidia huduma ya upimaji Malaria katika Hospitali ya Rufa ya Mkoa Geita.
Mkurugenzi wa Miradi taasisi ya APHFTA, Elizabeth Bonareri (kushoto), akimkabidhi Katibu Tawala Msaidizi Mkoa Geita, Herman Matemu (kulia) printa kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo. Mashine hiyo ni miongoni mwa vifaa tiba vilivyotolewa na taasisi ya APHFTA kuboresha huduma hospitalini hapo.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa Geita, Herman Matemu (katikati) akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Geita Mhandisi Robert Gabriel (hayuko pichani) baada ya kupokea vifaa tiba kutoka taasisi ya APHFA.
**
Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (APHFTA), leo kimekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya Tsh. Milioni 19 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Geita lengo likiwa ni kuboresha huduma ya upimaji Malaria kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Miradi APHFTA, Elizabeth Bonareri amesema vifaa hivyo ni pamoja na "Microscope" na kwamba chama hicho pia kimetenga Tsh. Milioni 30 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa jengo la maabara ya Hospitali hiyo.
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, Katibu Tawala Msaidizi, Herman Matemu amesema vifaa hivyo vitasaidia utoaji wa huduma bora kwa wananchi na hivyo kuomba vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mganga Mkuu mkoani Geita, Dkt. Japhet Simeo amesema juhudi mbalimbali ikiwemo kunyunyizia dawa ya ukoko majumbani, elimu sahihi kuhusu matumizi ya vyandarua vyenye dawa, utunzaji mazingira/ kufyekya nyasi na kufukia madimbwi pamoja na kuwahimiza wananchi kuwahi katika vipimo zimekuwa zikifanyika katika kupambana na ugonjwa wa Malaria ambapo pia ameishukru taasisi ya APHFTA kwa namna inavyoshirikiana na Serikali kupambana na ugonjwa huo.
Taasisi ya APHFTA kwa kushirikiana na kampuni ya Afya Micro-Finance kwa ufadhili wa wadau wa maendeleo "Comic Relief" inatekeleza mradi wa kupambana na Malaria mkoani Geita ambapo juhudi hizo zimesaidia kiwango cha maambukizi kupungua kutoka asilimia 38.1 mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 17 mwaka 2017/18.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG