Rais John Magufuli amesema viongozi wa Serikali waliokatiwa tiketi ili wasafiri na ndege za Shirika la ATCL na kukaidi watakatwa pesa hizo katika mishahara yao.
Ameyasema hayo leo Jumapili Desemba 23, 2018 wakati akipokea ndege mpya ya Airbus 220-300 ‘Dodoma’ katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya abiria wamekuwa wakikosa tiketi kwa kuambiwa ndege imejaa ila wanapoingia ndani hakuna watu huku baadhi ya tiketi zikiwa za watendaji wa Serikali ambao hawasafiri.
“Mtumishi anatakiwa kusafiri kwenye ndege na amekatiwa tiketi na Serikali lakini hasafiri na kufanya ndege iende tupu, nimeshamwambia mtendaji mkuu aniletee orodha ya watendaji ambao hawakusafiri tuwakate hizo hela kwenye mishahara yao,” amesema Rais Magufuli.
“Nimeambiwa wanakadiriwa kuwa 100 kwa hiyo nina uhakika kufika wiki ijayo nitapata majina yao, mawaziri, wabunge ambao walikaa hadi saa ya mwisho ndege ikaenda tupu na hela za Serikali zikaenda,” ameongeza Rais Magufuli huku akisema tena anafikiri kesho Jumatatu yatamfikia.
Amesema watumishi hao wajiandae kurudisha fedha hizo kutoka mifukoni mwao ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wanaotumia fedha za Serikali vibaya.
“Niwaombe tu watendaji kama kuna tiketi ambayo haukuitumia leta tu hela mara moja ili mambo yaishe lakini ni matumaini yangu sasa katika suala hili la tiketi ATCL mtajipanga vizuri,” amesema Magufuli.
Social Plugin