Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa ,Mkoa wa Pwani imemfikisha mahakamani Naziru Mwakangali aliyekuwa anafanya kazi kama kibarua katika mamlaka ya bandari Dar es salaam kwa makosa ya kuahidi kutoa rushwa ya sh.laki nne na kutoa rushwa ya kiasi cha shilingi 390,000,kinyume na kifungu cha 15(1)(b) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa na. 11 ya nwaka 2007.
Mwakangali alifunguliwa kesi ya jinai namba. 4 ya mwaka 2018 katika nahakama ya wilaya ya Mkuranga, Mkoani hapo.
Akisoma mashtaka mbele ya hakimu wa wilaya ya Mkuranga Tumsifu Barnabas, mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Euphrazia Kakiko ,aliieleza mahakama kwamba mshitakiwa alitenda kosa la kuahidi kutoa rushwa laki nne kwa mtoa taarifa ili ampatie ajira katika kiwanda cha Knauf Gypsum Tanzania Limited wilayani Mkuranga.
Aidha aliieleza ,mahakama kwamba nshitakiwa alitoa rushwa sh. 390,000 kwa mtoa taarifa, jambo ambalo pia ni kosa kisheria .Mshitakiwa alikiri kutenda makosa yote mawili, ambapo alitiwa hatiani na hivyo kupewa adhabu ya kutumikia kifungo jela kwa muda wa miaka mitatu kwa kila kosa ambapo mahakama iliamuru vifungo vyote viende pamoja ama kulipa faini ya sh. 500,000 kwa kila kosa kwa mujibu wa sheria ya kanuni za adhabu, sura ya 16 ya sheria za Tanzania.
Vilevile, mahakama iliamuru fedha zilizokamatwa kwa lengo la kutolewa na mshitakiwa kama rushwa zitaifishwe kuwa mali ya umma kwa mujibu wa sheria.Hata hivyo ,mshitakiwa alilipa faini kama Mahakama ilivyoelekeza.
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Suzan Raymond anatoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa na badala yake wafuate taratibu zinazotakiwa katika suala zima la utafutaji wa ajira
Social Plugin