Picha : WATOTO WA ARIEL CAMP 2018 WATEMBELEA MJI WA KIHISTORIA BAGAMOYO..WAKUTANA NA MAMBO YA AJABU


Watoto na vijana wanaoshiriki katika Kambi ya Ariel 2018 inayosimamiwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI)ambayo inafanyika jijini Dar es salaam wametembelea Makumbusho ya Kihistoria ya Mji wa Bagamoyo kwa ajili ya kujifunza historia ya nchi ya Tanzania tangu enzi za utawala wa wakoloni wa Kiarabu,Wajerumani na Waingereza.


Vijana na Watoto hao 50 kutoka mikoa ya Shinyanga,Mwanza,Simiyu na Mara wametembelea vivutio vilivyopo katika Mji maarufu wa Bagamoyo uliopo mkoani Pwani leo Desemba 13,2018 wakiwa wameongozana na walezi wao.

Miongoni mwa vituo vya kitalii walivyotembelea ni pamoja na Makumbusho ya kijiji cha Kaole  ambacho kinaelezwa kuwa karne ya 13 kilikuwa chini ya utawala wa Waajemi kutoka nchi za kiarabu.

Kijiji hicho kina kumbukumbu za kihistori za dini ya kiislam ambapo kuna Msikiti wa kale,makaburi ya Viongozi na watu maarufu pia Kaburi la Binti Sharrifa Sharifu aliyekuwa na nguvu za aina yake na alikufa akiwa na umri wa miaka 13 ambapo kwenye kaburi lake kumejengwa jengo linalofanana na msikiti huku pembeni kukiwa na makaburi ya watoto wachanga watatu. 

Wakiwa katika kijiji hicho, pia watoto na vijana hao wameshuhudia kisima chenye maji ya baraka ambacho kiko ndani ya msikiti wa kale,maji ya kisima hicho huwa hayaongezeki wala kupungua,pia kuna mbuyu wenye umri wa zaidi ya miaka 500 unaodaiwa ukiuzunguka unaongeza maisha ya watu.

Pia wamejionea Ngome Kongwe ya Bagamoyo, wakishuhudia maghofu,makaburi ya Wajerumani, sehemu ya kunyongea Waafrika waliokuwa wanapinga utawala wa Wajerumani na Makumbusho ya kanisa Katoliki ambapo ndipo kanisa mama/la kwanza lilipoanzia nchini Tanzania yapata miaka 150 sasa.

Angalia picha hapa chini
Mwongoza watalii,Daniel Msaky akielezea kuhusu maghofu ya Kaole washiriki wa Ariel Camp 2018. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Watoto na vijana wakiwa katika kaburi la Binti Sharrifa Sharifu aliyekuwa na nguvu za ajabu na alifariki akiwa na umri wa miaka 13 ambapo kwenye kaburi lake kumejengwa jengo linalofanana na msikiti. 
Watoto na vijana wakiwa katika makaburi ya viongozi na watu maarufu ambao ni Wahindi na Waarabu kutoka Iran Kusini waliofariki mwaka 1300. Eneo hili lina makaburi 22.

Mwongoza watalii,Daniel Msaky akionesha sehemu makaburi ya waislamu katika kijiji cha Kaole.

Kisima chenye maji ya baraka kilichopo katika kijiji cha Kaole ambacho kipo ndani ya msikiti wa kale. Inaelezwa kuwa maji ya kisima hicho huwa hayaongezeki wala kupungua,iwe kipindi cha mvua au jua. Hata uchote mara nyingi maji hayapungui,yapo vile vile.
Watoto wakichota maji katika kisima chenye maji ya baraka. Inadaiwa ukioga/ukinawa maji hayo mikosi uliyonayo inaondoka.
Washiriki wa Ariel Camp wakichukua maji ya kisima cha maji ya baraka.
Washiriki wa Ariel Camp wakiwa katika Bandari ya zamani katika kijiji cha Kaole.
Washiriki wa Ariel Camp 2018 wakiwa katika mbuyu wenye umri wa zaidi ya miaka 500. Inaelezwa kuwa ukiuzunguka unaongeza umri wako wa kuishi duniani. Huu ni miongoni mwa mibuyu yenye umri mkubwa zaidi nchini Tanzania. Eneo hili lilitumika kwa shughuli za matambiko na kuabudu.
Washiriki wa Ariel Camp 2018 wakizunguka mbuyu huo ili kuongeza umri wao.
Washiriki wa Ariel Camp wakiwa katika jumba la makumbusho katika kijiji cha Kaole.
Hapa ni eneo la Ngome Kongwe Bagamoyo : Mwongoza Watalii, Gadafi Mbia Nang'uto akiwaelezea washiriki wa Ariel Camp 2018 kuhusu utawala wa Wajerumani,Waingereza na biashara ya watumwa.

Mwongoza Watalii, Gadafi Mbia Nang'uto akionesha majengo yenye umri wa zaidi ya miaka 100 yaliyokuwa yanatumiwa na Wajerumani na Waingereza katika mji wa Bagamoyo.
Sehemu hii ya juu ya jengo ilikuwa inatumiwa na askari wa Kijerumani kujificha na kuhifadhi silaha.
Washiriki wa Ariel Camp wakiwa juu ya majengo yenye umri wa zaidi ya miaka 100 katika Ngome Kongwe Bagamoyo.

Washiriki wa Ariel Camp wakiwa ndani ya moja ya majengo ambayo hayajaharibika yapata miaka 100 sasa katika mji wa Bagamoyo 'Ngome Kongwe Bagamoyo'. Jengo hili lilikuwa linatumika kuhifadhia watumwa.
Mwongoza Watalii, Gadafi Mbia Nang'uto akionesha mlango wa ajabu uliopo katika ngome kongwe ya Bagamoyo. Jengo hilo pia lilitumika kama Chuo cha watumwa,gereza kuu na makao makuu ya polisi.
Hii ni sehemu iliyotumika kunyonga Waafrika waliokuwa wanapinga utawala wa Wajerumani.
Mwongoza Watalii, Gadafi Mbia Nang'uto akionesha moja ya makaburi ya Wajerumani waliouawa wakati wa vita dhidi ya Wajerumani na Abushiri Ibn Salim al-Harthi aliyekuwa kiongozi wa upinzani dhidi ya ukoloni wa Wajerumani mnamo mwaka 1889.
Mwongoza Watalii, Gadafi Mbia Nang'uto akionesha moja ya makaburi ya Wajerumani waliouawa wakati wa vita dhidi ya Wajerumani na Abushiri Ibn Salim al-Harthi.
Washiriki wa Ariel Camp wakiwa katika Ikulu ya Wajerumani 'Germany Boma Bagamoyo'.
Mwongoza watalii,Daniel Msaky akielezea ikulu hiyo ya Wajerumani.
Washiriki wa Ariel Camp wakiwa katika Soko la Watumwa ambalo sasa ni soko la vifaa vya sanaa.
Washiriki wa Ariel Camp wakiendelea kutembelea mji wa Bagamoyo.
Washiriki wa Ariel Camp 2018 wakiwa katika mnara kwenye Makumbusho ya kanisa katoliki.Inaelezwa kuwa hapa kuna kanisa mama la kanisa katoliki nchini Tanzaania.
Sehemu ya Kanisa Mama la Makanisa yote Katoliki nchini Tanzania lililojengwa mwaka 1872.
Washiriki wa Ariel Camp 2018 wakiwa katika mbuyu wenye umri wa miaka 150 uliopandwa mwaka 1868 na Padre Anthony Horner kwa ajili ya kumbukumbu ya ufunguzi wa Misheni ya Katoliki ya Bagamoyo.
Mwongoza watalii,Gadafi Nang'uto akionesha mnyororo uliopo katika mbuyu uliopo katika kanisa katoliki la kwanza nchini Tanzania. Mnamo mwaka 1895 muuguzi wa kujitolea,Madame de Chevalier aliyekuwa akifanya kazi katika zahanati ya Zanzibar alifika Bagamoyo kuwasaidia Wamisionari kazi za uuguzi katika hospitali ya Misheni.Aliufunga mnyororo huo katika mbuyu na aliutumia kumfungia punda wake wakati akija kazini.Kutokana na kukua kwa mbuyu sehemu kubwa ya mnyororo imemezwa,pingili moja inayoonekana kwa mbali sana ni sehemu ya mnyororo huo iliyobaki.Mwaka 2012 pingili 34 ziliongezwa ili kuendeleza historia. 
Hapa ni katika jumba la makumbusho ya kanisa katoliki Bagamoyo : Mwongoza watalii,Gadafi Nang'uto akionesha kidude kilichokuwa kinatumika kuhifadhia pesa.
Mtoto akiangalia kifaa cha kuchujia maji kilichotengenezwa kwa mawe ya baharini.
Kijana akipiga picha ya kumbukumbu ndani ya makumbusho ya kanisa katoliki Bagamoyo.
Washiriki wa Ariel Camp wakiwa katika jumba la makumbusho ya kanisa katoliki Bagamoyo.
Washiriki wa Ariel Camp wakiwa ndani ya makumbusho ya kanisa katoliki.
Vijana wakiangalia vitu vya kale ndani ya jumba la makumbusho ya kanisa katoliki Bagamoyo.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم