Kampuni ya Altria, ambayo ni wazalishaji wa chapa maarufu ya sigara za Marlboro wapo katika mazungumzo na kampuni moja ya kuzalisha bangi nchini Canada ili wawekeze mtaji wao.
Kampuni ya Cronos imethibisha kuwa katika mazungumzo na Malboro ambayo inataka kuinunua ili kuingia rasmi kwenye biashara ya bangi.
Canada iliruhusu kisheria uvutaji wa bangi kama starehe mwezi wa Oktoba mwaka huu, ni nchi ya pili kufanya hivyo baada ya Uruguay.
"Tupo kwenye mazungumzo, kampuni ya Altria inataka kuwekeza kwenye kampuni yetu ya Cronos. Bado hatujafikia makubaliano, na hakuna uhakika kwa sasa kama uwekezaji utafanyika," imesema taarifa ya Cronos.
Tayari makampuni kadhaa duniani yameanza kuweka mipango ya kuwekeza kwenye sekta ya bangi.
Wazalishaji wa bia ya Corona, kampuni ya Constellation Brands imesema itawekeza dola bilioni 4 kwenye kampuni kubwa zaidi ya uzalishaji bangi nchini Cananda, Canopy Growth. Uwekezaji huo ndio mkubwa zaidi mpaka sasa katika biashara ya bangi duniani.
Kampuni maarufu ya vinywaji ya Coca-Cola ni maarufu zaidi kwa kutengeneza soda, lakini sasa inapanga kufanyia majaribio aina mpya ya kinywaji ambacho kitakuwa na bangi.
Chanzo:Bbc
Social Plugin