HOTUBA YA MHE. UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO WAKATI WA UZINDUZI WA BARAZA JIPYA LA FAMASI KATIKA UKUMBI WA WIZARA TAREHE 17 NOVEMBA, 2018
Mwenyekiti wa Baraza la Famasi uliyemaliza muda na wa sasa;
Wajumbe wa Baraza la Famasi waliomaliza muda na wanaoingia kazini;
Wakurugenzi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee;
Msajili wa Baraza la Famasi;
Wasajili kutoka Bodi na Mabaraza chini ya Wizara;
Watumishi wa Wizara pamoja na Sekretarieti ya Baraza;
Wageni waalikwa;
Wanahabari;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutukutanisha siku hii ya leo. Pili nitoe shukrani zangu za dhati kwa kunipa nafasi ya kukutana na kuzungumza pamoja nanyi na kuzindua Baraza Jipya la Famasi ambalo ni la awamu ya nne (4) tangu Baraza hili kuanzishwa rasmi mwaka 2003.
Aidha, nichukue nafasi hii kwa niaba yangu binafsi na ya Wizara kuupongeza uongozi wa Baraza chini Mwenyekiti Ndugu Legu Mhangwa kwa moyo wa kujitolea na kufanya kazi nzuri pamoja na changamoto zilizokuwepo. Ni ukweli usiofichika kwamba mmefanya kazi nzuri katika kulijenga Baraza la Famasi.
Nimesikiliza kwa makini mafanikio mbalimbali ambayo Baraza limeyapata kufuatia maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake pamoja na Msajili wa Baraza na kwamba, pamekuwepo na umuhimu wa kufanya mapitio ya kanuni na miongozo mbalimbali ambayo imeonekana imepitwa na wakati ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sasa.
Katika muda wa miaka mitatu (3) mliyotumika, Baraza limeonyesha uwezo mkubwa wa kudhibiti taaluma na wanataaluma, kusimamia na kudumisha maadili na miiko ya taaluma ya famasi, pamoja na usimamizi wa utoaji wa huduma za dawa na hivyo kuendeleza na kuboresha uhai wa fani ya famasi.
Pamoja na maboresho hayo niwapongeze kwa kupandishwa hadhi kwa Baraza na kuwa taasisi inayojitegemea. Hii inaonesha jinsi mlivyoweza kuweka juhudi katika kujisimamia na kuongeza ufanisi kiutendaji katika majukumu yenu. Kwa kuwa baadhi yenu mmemaliza wajibu wenu leo, ninawasihi kutokana na uzoefu mlioupata katika kipindi cha miaka mitatu, muendelee kutoa ushauri kwa wajumbe wapya ambao wanakabidhiwa majukumu haya ili kufanikisha malengo na madhumuni ya kuwepo kwa Baraza hili.
Mabibi na Mabwana,
Kwa moyo wa dhati nawapongeza wajumbe wapya ambao mnakabidhiwa majukumu hivi leo, Wizara yangu na Serikali kwa ujumla tuna matarajio makubwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu (3) ambacho mtakuwa na jukumu hili kubwa la kuishauri Wizara katika mambo kadha wa kadha ya taaluma hii na hatimaye kuboresha utoaji wa huduma za dawa katika vituo na sehemu mbalimbali zinazofanya shughuli hizi kwa mujibu wa Sheria.
Mabibi na Mabwana,
Ni imani yangu kubwa kuwa wengi wenu katika Baraza lililotangulia na hili la sasa mnafahamu fika majukumu yenu kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Famasi, Sura 311 inayounda Baraza hili. Sitakuwa na sababu ya kuyataja, ila nashauri muweze kurejea kwenye sheria hiyo ambayo katika hayo nisisitize kushirikiana na taasisi mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine zinagusa masuala ya taaluma hii ikiwa ni pamoja na mafunzo ya wanataaluma wa fani hii ili kutosababisha migongano ya kiutendaji ya ndani na nje ya Wizara zinazohusika.
Mabibi na Mabwana,
Pamoja na kazi nilizozitaja hapo juu, jukumu la Baraza la Famasi ni kuleta msukumo wa utoaji huduma bora ya afya kwa mtanzania. Hili linawezekana kwa kuhakikisha kuwa wanataaluma wanazingatia maadili na nidhamu ya taaluma katika ununuaji, utunzaji na matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba vilivyo salama na ubora wa hali ya juu.
Vile vile, napenda nisisitize kuwa Baraza lione umuhimu wa kuweka msukumo wa pekee kwenye masuala ya kuboresha mafunzo na elimu ili tuwe na wanataaluma wenye uwezo wa utendaji wa kiwango cha hali ya juu katika nchi yetu katika maeneo yote ikiwamo uzalishaji wa dawa Viwandani ili kwenda sambamba na adhima ya Serikali kuelekea uchumi wa Viwanda.
Mabibi na Mabwana,
Napenda kuwahakikishia kuwa, jamii ya watanzania wanahitaji huduma hii, hali inaonesha kuwa, kupitia takwimu mbalimbali zaidi ya 40% ya wananchi wanapopata tatizo la afya huanza kwenda kupata huduma ya awali kwenye maduka ya dawa (famasi na maduka ya dawa muhimu), hivyo basi kushindwa kuwa na huduma bora katika maeneo hayo na inahatarisha kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi.
Wizara inalitambua hili na umuhimu wa kuwepo kwa fani hii hapa nchini. Kwa kushirikiana na kada nyingine za afya huduma za afya zitaendelea kuboreka na kuthaminiwa katika maeneo yetu ya kazi.
Mabibi na Mabwana,
Wataalam wa fani ya famasia ndio wahusika wakuu katika masuala yote yanayohusu dawa katika kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana katika hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini. Serikali kwa upande wake imeongeza bajeti ya Dawa kutoka Shilingi bilioni 30 mwaka 2015/2016 hadi Tsh 270 Bilioni mwaka 2018/2019, hivyo ni Wataalamu hawa wa Famasi wanaotakiwa kuhakikisha kuwa ongezeko la bajeti linaenda sambamba na upatikanaji wa dawa na matumizi sahihi kwa kuzingatia miongozo ya tiba. Ni dhahiri kuwa utaalamu wa kutengeneza, uagizaji, usafirishaji, usambazaji, utoaji dawa sahihi kwa wagonjwa, utunzaji na utoaji mafunzo yahusuyo dawa ndiyo msingi mkubwa wa taaluma hii. Hivyo basi Baraza ambalo ndilo lililopewa dhamana ya kusimamia kazi za utendaji wa taaluma hii kuongeza nguvu za usimamizi na udhibiti wa sheria na miongozo na kuhakikisha kazi za wataalamu hawa zinafuata miiko na taratibu za kitaaluma zilizowekwa na zinafanyika kwa uangalifu; na kuchukua hatua zinazostahili pindi inapogundulika kuna ukiukwaji wa Sheria na taratibu
Pia ni wajibu wa wanataaluma kuwa mfano mzuri kwa jamii wanayoihudumia ili kujenga imani na kudumisha uhusiano mzuri na jamii wanazozihudumia.
Wageni Waalikwa,
Kuhusu migogoro ambayo nimekuwa nikiisikia kati ya Baraza na Wafanya biashara wa Maduka ya Dawa ni vyema tuchukue hatua za haraka ili kuondoa changmoto hizo na katika hili naelekeza Baraza tufanya yafuatayo:
Maduka ya Dawa yasiyo na vibali yaliyopo katika maeneo yasiyoruhusiwa kuendesha maduka ya ADDO, kwa sasa yapewe muda wa mpito wa miaka miwili (2) kuanzia tarehe ambayo utatoa taarifa hiyo kwa umma;
Katika kipindi hicho maduka hayo yauze dawa zisizohitaji cheti cha Daktari (general sales medicines) kwa utaratibu ambao utaandaliwa na Baraza la Famasi kwa masharti kwamba endapo watakiuka utaratibu huo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao;
Baada ya muda huo kupita, maduka haya yatatakiwa aidha kufungwa, kupandishwa hadhi kuwa Famasi au kuhamia maeneo yanyoruhusiwa ADDO na kuendelea kutoa huduma hiyo; na
Wamiliki wa Maduka ya Dawa ambayo yapo katika maeneo yanayoruhusiwa kuendesha ADDO wayapandishe hadhi maduka yao mara moja.
Mabibi na Mabwana,
Napenda kuwahakikishia kuwa yote yatawezekana kama sisi sote tutakubaliana kusimamia na kutekeleza suala la uwazi na ukweli (Transparency & Good Governance). Nawasihi kuendelea kushirikiana na nchi nyingine ili kupata uzoefu zaidi wa namna bora ya kusimamia taaluma hii ya Famasia.
Hitimisho,
Mwisho ningependa kuwahakikishia kwamba Wizara ipo tayari kuwasaidia katika mipango iliyopo na ile mtakayoipendekeza kwa serikali kulingana na hali halisi ya uwezo. Niwatakie Baraza jipya linalozinduliwa leo utekelezaji mzuri wa majukumu yenu.
Baada ya kusema hayo machache, sasa natamka kuwa Baraza la Famasi limezinduliwa rasmi.
Asanteni kwa Kunisikiliza.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akimkabidhi zawadi mmoja kati ya Wajumbe wa Baraza la Wafamasia wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la Famasia leo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam
Social Plugin