Dr. Ellyson Maeja
Uongozi wa klabu ya Stand United ya mkoani Shinyanga umepanga kulishtaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokana na hatua yake ya kumruhusu aliyekuwa mchezaji, Bigirimana Blaise, kusajiliwa na timu ya Alliance FC ya Mwanza.
Mwenyekiti wa Stand United, Dk. Ellyson Maeja, alisema klabu yake bado inatambua mchezaji huyo wana mkataba naye, hivyo hatua ya TFF kumwidhinisha Alliance wao wametafsiri kama uonevu.
“Tunasikitishwa na kitendo cha TFF kumruhusu Bigirimana kuitumikia Alliance wakati Stand United tayari imewasilisha malalamiko, nasisitiza kwamba sisi hatujampa barua ya kumruhusu kuondoka.
“Kwa kawaida na jinsi mfumo ulivyo mchezaji haruhusiwi kusajiliwa na timu nyingine, lazima kwanza aandikiwe barua na uongozi wa kule alikokuwa anachezea awali na wenye mamlaka ya kutoa barua ya ruhusa ni kiongozi wa TFF au kiongozi wa timu yake ya kwanza?” alihoji Dk. Maeja.
Bigirimana alikuwa sehemu ya kikosi cha Alliance ambacho kililazimishwa sare ya bao 1-1 na Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Katika mchezo huo uliopigwa Ijumaa iliyopita, Alliance FC ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya 24 lililofungwa na Dickson Ambundo kabla ya Musa Hafidh kuisawazishia Stand United dakika ya 89.
Sam Bahari - Shinyanga
Social Plugin