KIGOGO WA CHADEMA AKAMATWA NA POLISI AKIJIANDAA KUSHIRIKI KIKAO


  Jeshi la Polisi mkoani Iringa limemkamata Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu.

Mwalimu amekamatwa leo Jumapili Desemba 16, 2018 Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa akiwa anajiandaa kushiriki kikao cha ndani cha chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

Jeshi la Polisi mjini Mafinga, mkoani Iringa, linamshikilia Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA-Zanzibar, Salum Mwalim baada ya kumkamata mchana wa leo Desemba 16, 2018 alipokuwa akiwasili kuongoza kikao cha ndani cha chama mjini hapo.

Tukio la kukamatwa kwa Naibu Katibu Mkuu Mwalim lilitanguliwa na kitendo cha askari takriban saba kumfuata na kumtoa ndani ya gari kwa nguvu bila kutoa maelezo yoyote ya sababu ya kufanya hivyo.

Hapo awali, takriban polisi 40 waliokuwa kwenye magari matatu wakiwa na silaha za moto walifika Ukumbi wa Mamu ambapo maandalizi ya kikao hicho cha ndani yalikuwa yanaendelea, wakisema kuwa wameagizwa kuzuia kikao hicho na Mkuu wa Wilaya.

Hadi tunapotoa taarifa hii, askari polisi bado wako katika eneo la kikao hicho Ukumbi wa Mamu, Mafinga mjini. 

Wengine waliokamatwa pamoja na NKMZ Mwalim ni, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Iringa, Jackson Mnyawami na Jailos Mwaijande, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) Mbeya mjini, Jailos Mwaijande. Wote wanashikiliwa Kituo cha Polisi Mafinga hadi sasa.

Tunalaani na kukemea vikali kitendo cha Jeshi la Polisi kumkamata NKMZ Mwalim akiwa na viongozi wengine na kumtendea kama mhalifu. Mwendelezo huu wa vitendo vya askari wa jeshi hilo kuvunja sheria za nchi na kuwanyanyasa viongozi wa upinzani nchini haukubaliki na unazidi kuchochea hisia kali za uonevu katika jamii.

Tunalitaka Jeshi la Polisi kutoa taarifa rasmi juu ya tukio hilo na kuhakikisha NKMZ Salum Mwalim na viongozi wengine waliokamatwa wanapata stahiki zao kwa mujibu wa sheria kama raia wasiokuwa na hatia, ikiwemo kuwaachia huru mara moja.

Imetolewa leo Jumapili, Desemba 16, 2018 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post