Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Zanzibar), Salum Mwalimu.
Baada ya Polisi mjini Mafinga mkoani Iringa Jumapili ya Disemba 16, kumkamata na baadaye kumwachia, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Zanzibar), Salum Mwalimu, mwenyewe amefunguka kuwa kilichofanyika ni uonevu dhidi ya demokrasia.
Akizungumza na www.eatv.tv, Mwalimu amesema kuwa kinachodaiwa na aliyetoa agizo la kukamatwa kwake kuhusiana na kutokuwa na kibali cha kufanya mkutano wa ndani hakikuwa sahihi kwa mujibu wa sheria.
Mwalimu amesema kitendo alichofanyiwa kilikuwa cha udhalilishaji na uonevu kwani, hakuwa na kosa lolote ambalo alitenda na kuongeza kuwa hata mikutano ya hadhara ya kisiasa huwa hakuna kibali bali taarifa.
"Sisi sio wajinga kuwa tunavunja sheria makusudi, kama sheria hiyo ipo tungeifuata kama tunavyofanya kwingine, nimekamatwa, nimepigwa na kudhalilishwa bila sababu za msingi", amesema Mwalimu.
Salum Mwalimu alikamatwa wakati akijiandaa kushiriki kikao cha ndani cha chama hicho, na baadaye kuachiwa bila masharti yoyote kutoka kwa Jeshi la Polisi.
Chanzo- EATV
Social Plugin