Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAFUNZI 133,747 WALIOFAULU DARASA LA SABA WAKOSA NAFASI KIDATO CHA KWANZA 2019

Wanafunzi 133,747, sawa na asilimia 18.24 ya waliofaulu mtihani ya darasa la saba mwaka huu hawajapata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alibainisha changamoyo hiyo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga kidato cha kwanza mwakani.

Jafo alisema kuwa, kati ya wanafunzi hao, 62,808 ni wavulana na 70,939 ni wasichana.

Aliitaja mikoa yenye uhaba wa vyumba vya madarasa na idadi ya wanafunzi waliokosa nafasi kuwa ni Arusha (18,719), Dodoma (5,991), Iringa (2,774), Kagera (14,046), Kigoma (12,178), Lindi (1,294), Mara (16,356).

Mingine ni Mbeya (6,395), Pwani (4,731) Rukwa (4,930), Tabora (11,209), Tanga (5,400), Manyara (5,392), Shinyanga (6,271), Katavi (1,249), Njombe (3,172) na Simiyu (12,684).

Jafo alisema jumla ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani ni 599,356, sawa na asilimia 81.76 ya wanafunzi 733,103 waliofaulu.

“Nawashukuru walimu, walimu wakuu, kamati za shule, maofisa elimu kata, viongozi wa mikoa na halmashauri na wadau wote wa elimu kwa kutoa ushirikiano katika kusimamia uendeshaji na utoaji wa elimu bora nchini,” alisema.

Jafo aliagiza walimu na watendaji wa elimu katika ngazi zote kuongeza bidii katika usimamiaji, ufuatiliaji na utoaji wa elimu ili kuboresha hali ya elimu nchini.

Waziri huyo pia aliziagiza halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa elimu kukamilisha majengo na kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwezi ujao bila kuwapo vikwazo vya aina yoyote.

“Pasiwapo vikwazo vya aina yoyote ikiwamo michango na ada ili kutekeleza sera ya utoaji wa elimu msingi bila malipo," alisema Jafo.

Aliagiza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza ikiwa ni pamoja na kufanya ufuatiliaji shuleni ili kubaini changamoto mbalimbali na kuzitatua kwa haraka.

Jafo aliagiza mikoa na halmashauri zilizobakiza wanafunzi waliofaulu kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwawezesha wanafunzi hao kujiunga na kidato cha kwanza kabla ya mwisho wa Februari mwakani.

Alisema mikoa tisa ndiyo yenye mazingira mazuri ya miundombinu ya kuwawezesha wanafunzi wao wote kujiunga na elimu ya sekondari.

“Mikoa 17 ina milolongo ya idadi ya vyumba vya madarasa, hivyo idadi ya wanafunzi ukiigawa katika uwiano, hawatoshi katika madarasa,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com