DIAMOND AZOZANA NA SHIRIKA LA NDEGE TANZANIA KISA KUACHWA NA NDEGE UWANJANI

Mwanamuziki nyota kutoka Tanzania Diamond Platnumz ametofautiana na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuhusu kilichotokea hadi akaachwa na ndege uwanjani Mwanza.

Mwanamuziki huyo anasema tamko lililotolewa na shirika hilo kwamba alichelewa kufika uwanjani si za kweli.

ATCL kupitia taarifa wamesema Diamond , ambaye wamemrejelea kama Isaack Nasibu, alikuwa miongoni mwa abiria waliopaswa kusafiri na ndege ya shirika hilo Jumapili 16 Desemba, 2018 hakuachwa kama inavyodaiwa bali alichelewa kufika uwanjani kwa muda unaotakikana.

Anadaiwa kufika dirishani robo saa baada ya dirisha kufungwa.

Jina rasmi la mwanamuziki huyo ni Nasibu Abdul Juma Issaack.

"Kampuni inapenda kutoa ufafanuzi kuwa abiria huyo alifika uwanjani kwa kuchelewa na hivyo kuzuiliwa na mamlaka zinazosimamia uwanja kwa mujibu na taratibu," ATCL wamesema.

Aidha, shirika hilo la serikali limepuuzilia mbali madai ya msanii huyo kwamba tiketi yake iliuzwa kwa abiria wengine.

"Kampuni inapenda kutoa ufafanuzi kwamba, tuhuma hizo si za kweli kwani tiketi za kampuni yetu zinamruhusu mteja wetu kuitumia tiketi yake ambayo haijatumika kwa siku nyingine ambapo atakuwa tayari kusafiri nasi.

"Hata hivyo mteja wetu aliyelalamika ameiomba kampuni kutumia tiketi yake siku ya leo.

"Kampuni ya ndege Tanzania (ATCL) imesikitishwa na tuhuma na malalamiko yaliyotolewa na ndugu Issaack Nasibu na wenzake kwa kupitia video waliyojirekodi na kuirusha kwenye mitandao ya kijamii wakati kampuni inazo taratibu za namna ya kuwasilisha malalamiko pindi mteja asiporidhika na huduma zetu."

ATCL wametoa wito kwa abiria "kuzingatia muda unaoonyeshwa katika tiketi zao ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima."

Mkuu wa mawasiliano wa shirika hilo Josephat Kagirwa amesema shirika lililazimika kutoa ufafanuzi kwa umma baada ya kuona malalamiko ya Diamond yakisambaa katika mitandao ya kijamii.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond amesema hakuchelewa kamwe na badala yake akadai kuna mchezo ulifanyika ikiwa ni pamoja na tiketi za abiria kuuzwa kwa abiria wengine, ambapo anasema miongoni mwa waliokuwa wanauziwa ni baadhi ya wafanyakazi wa kampuni yake ya Wasafi Media.

Licha ya kwamba ujumbe ni wa kulalamika, kwenye picha yake ameweka picha ya ndege ya Air Tanzania na kitambulisha mada #WakwanzaAfrika, kuashiria kwamba shirika hilo litakuwa la kwanza Afrika kupokea ndege aina ya Airbus A220-300.

"Sikuchelewa ndege Kabisa..Nilifika muda sawia kama usafiri wa ndege za ndani unavyotaka, na kulidhihirisha hilo.. nikiwa niko pale kuna hata abiria wengine waliingia nusu saa baadae, tena nikiwepo nimesimama palepale..." ameandika kwenye Instagram.
".. na mmoja ya watu waloingia nikiwepo nimesimama ni @Harmonize_tz ..."

"Kilichotokea ni kuwa Mmoja ya watu wenye dhamana pale, siti zetu (viti vyetu) aliziuza kwa abilia (abiria) wa fastjet...kwa abiria watalii wazungu, na walichokuwa hawajajua pia waliwauzia na baadhi ya watu ambao ni wafanyakazi wetu wa Wasafi Media..."

"Na Kuthibitisha tena kuwa hatukuchelewa, alikuja tena mtu wa Air Tanzania na kutuambia kuwa siti zimebaki mbili...Hivyo tuchague watu wawili tu wasafiri....

"Kama kweli tulichelewa, sasa hao wawili, sasa wangewezaje ingia??? tukasema hatuwezi safiri wawili lazima tuwe wote kama tulivyokata... hivyo ni dhahiri kuwa hatukuchelewa....ila kutokana na Ndege nyingi za kuja mwanza zilicancel trip zao, ikiwepo Fastjet hivyo tickets zikawa ni dili sana na ndio yote kutokea...."

Ametetea msimamo wake na kusema „ kama Mtanzania Mzalendo Mwenye akili Timamu, siwezi tu kukurupuka kusema jambo kwani ni jukumu langu kuhakikisha nalilinda shirika hili."

"Nikiwa kama Mtanzania mwenye uchungu siwezi kuona mtu alopewa dhamana ya kuzisimamia ndege hizo anafanya vitu tofauti halafu eti nikakaa kimya..."

Harmonize, mwanamuziki mwenzake, ameandika maoni kwenye ujumbe wa Diamond na kusema 'Fact', kwa Kiingereza kwa maana ya kweli kabisa.
ATCL wanasema nini kilitokea?

Kwa mujibu wa shirika hilo la ndege, abiria Issaack Nasib aliyekuwa na tiketi namba- 197 2400458865 ya kampuni ya ndege ya Tanzania alikuwa katika safari ya kutoka Mwanza kwenda Dar Es Salaam, ndege nambari TC103 ya jioni tarehe 16 Disemba 2018. Kwa kawaida shirika hilo linasema abiria hutakiwa kufika uwanjani masaa mawili kabla ya ndege kuruka.

ATCL wanasema afisi yao ya Mwanza ilifungua dirisha kwa ajili ya kuwahudumia wateja (wasafiri) majira ya 17:45 na kulifunga majira ya 20:00.

Ndege hiyo iliruka kutoka Mwanza kuja Dar Es Salaam majira ya saa 20:45 na kuwasili Dar Es Salaam saa 22:00.

"Kwa kumbukumbu zilizopo kwa kutumia vyanzo mbalimbali, zikiwemo Camera (CCTV) za uwanjani inaonekana abiria tajwa hapo juu alifika majira ya 20:15 ambapo dirisha lilikuwa limeshafungwa. "

Bw Kagirwa, akizungumza na wanahabari alisema: "Tiketi ya mteja haiwezi kuuzwa. Ila asipoonekana uwanjani na akawepo mtu mwingine anahitaji huduma tutampa nafasi maana nafasi katika ndege thamani yake inaisha ndege inaporuka lakini tiketi baada ya hapo inabadilishwa."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم