DRC: UPINZANI WAONYA DHIDI YA KUAHIRISHA TENA UCHAGUZI

Muungano wa kisiasa unaomuunga mkono mgombea wa upinzani Felix Tshisekedi umemshutumu Rais Joseph Kabila kukosa dhamira ya kuandaa uchaguzi na kuondoka madarakani, lakini ukawataka wafuasi wao kuendelea kuwa watulivu.



Muungano huo ujulikanao kama CACH, umeonya kwamba hauwezi kuvumilia kuahirishwa kwingine kwa uchaguzi, hata kwa siku moja baada tarehe mpya iliyotangazwa na tume ya uchaguzi, tarehe 30 Desemba.

Mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu pia ametoa tamko kama hilo la muungano wa CACH, akisema hatua za kuendelea kuchelewesha uchaguzi haziwezi kuvumiliwa, na kuwabebesha lawama kikamilifu Rais Kabila na Mkuu wa tume ya uchaguzi, Corneille Nangaa. 


Tangazo la Fayulu limetiwa saini na vigogo wawili wa kisiasa waliozuiliwa kugombea, gavana wa zamani wa jimbo la Katanga Moise Katumbi, na aliyekuwa kiongozi wa waasi, Jean Pierre Bemba.


Na katika makala iliyoandikwa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Dakta Denis Mukwege na kuchapishwa katika gazeti maarufu la New York Times la nchini Marekani, Mukwege amemtaka Kabila na wale aliowaita vibaraka wake mafisadi, kukabidhi madaraka, akionya juu ya uwezekano wa kuzuka ghasia kubwa ikiwa wataendelea kung'ang'ania uongozini.


Mkwege amesema kuna haja ya dharura nchini Kongo ya kupata serikali ya wataalamu, ambayo itaipa nchi mwelekeo na kuandaa uchaguzi wa kuaminika.


Huku haya yakijiri, juhudi za tume ya uchaguzi, CENI zimepata pigo, baada ya ndege aina ya Antonov iliyokodiwa na tume hiyo kusafirisha karatasi za kura, kuanguka karibu na mji wa Kinshasa jana jioni, ilipokuwa ikirejea katika mji mkuu kutoka katika mji wa katikati ya nchi wa Tshikapa, ambako ilikuwa imepeleka vifaa vya uchaguzi.


Kuna taarifa zinazotofautiana kuhusu idadi ya waliokufa katika ajali ya ndege hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Gomair. Afisa wa ukaguzi wa safari za ndege katika uwanja wa ndege wa Tshikapa, amesema ndani ya ndege hiyo walikuwemo wahudumu 5 na msafiri mmoja, na kwamba wote wameuawa.


Lakini balozi wa Urusi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Alexei Senteboff, amenukuliwa na mashirika ya habari akisema ndege hiyo ilikuwa na wafanyakazi watatu, wote raia wa Urusi, na wote wamekufa. 


Alisema kwamba awali kulikuwepo taarifa ambazo hazikuthibitishwa, zilizodai kwamba walikuwemo watu 23 ndani ya ndege iliyoanguka, wakiwemo wafanyakazi watatu raia wa Urusi.


Hadi sasa hakuna ripoti zozote za machafuko, kufuatia tangazo la CENI la juzi jioni, la kuahirisha kwa wiki moja uchaguzi uliotarajiwa kufanyika kesho Jumapili.


Credit:DW

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post