MAMLAKA YA SAFARI ZA ANGA TCAA YATANGAZA KUIFYEKELEA MBALI FASTJET KUFANYA KAZI TANZANIA



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya safari za anga Tanzania (TCAA) , Hamza Johari akitangaza notisi ya siku 28 ya kusudio la kusitisha leseni ya kampuni ya FastJet kutoa huduma za usafiri wa anga Tanzania.
Wanahabari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya safari za anga Tanzania (TCAA) , Hamza Johari wakati akitoa ufafanuzi juu ya notisi ya siku 28.
Wanahabari wakiuliza maswali.


Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

Mamlaka ya safari za anga Tanzania (TCAA), imetangaza kuwa kampuni ya ndege ya Fastjet imepoteza sifa za kufanya biashara nchini. TCAA imetoa notisi ya siku 28 ya kusudio la kusitisha leseni ya kampuni ya kutoa huduma za usafiri wa anga Tanzania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema kuwa kwa sasa wameamua kuwapa notisi ya siku 28 ili waweze kujipanga upya kama wanaweza kuendelea na biashara au imeshawashinda kutokana na mwenendo mzima wa biashara wanavyoiendesha.

Amesema kuwa Fastjet limepoteza sifa ya kufanya biashara nchini, na wameizuia ndege moja waliyonayo kuruka kutokana na matatizo ya mara kwa mara na kukosekana kwa meneja mwajibikaji wa shirika.

"Tumekuwa tukiwaandikia barua ya kuwataka watueleze kuhusu mwenendo wao wa biashara tangu Fastjet Plc wajiondoe lakini pia shirika limekuwa na madeni mbalimbali ambayo hayajalipwa. Tukiomba watupe mpango wao wa fedha na biashara kwa mujibu wa sheria hawafanyi hivyo," amesema Johari.

Amesema shirika hilo linadaiwa na watoa huduma wake wengi ikiwemo TCAA inayolidai Sh1.4 bilioni lakini pia halina meneja mwajibikaji ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ndege anayepaswa kutoa majibu ya hali ya ndege.

"Kwa sasa fastjet hawana ndege. Ndege yao tangu jana tumeizuia kuruka kwa kuwa imekuwa ikipata hitilafu mara kwa mara na hawana mtu ambaye anaweza kutoa taarifa kuhusu mwenendo wake jambo ambalo linahatarisha usalama endapo itaruka," amesema Johari.

Amewaomba wananchi kuepuka kutapeliwa na wale watoa huduma watakaowakatia tiketi za Fastjet wakati hazifanyikazi kwa sasa, hawana ndege wameyumba.

Mapema leo FastJet imesimamisha safari zake zote na tayari imetangaza kuanzia Desema 20, kuwarudishia nauli kwa abiria waliokuwa wasafiri Disemba na Januari mwaka huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم