WANAUME WA KANDA YA ZIWA WAHAMASISHWA KUFANYA TOHARA KINGA

Pamoja na madhara ya kiafya yanayojitokeza kwa mwanaume ambaye hajafanyiwa tohara kinga iliyo salama,ikiwa ni pamoja na kuwa hatarini kupata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi, magonjwa ya zinaa pamoja na kupata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,baadhi ya jamii zinazopatikana katika mikoa ya Kanda ya ziwa zimetajwa kutothamini suala la tohara.

Pia baadhi ya makabila yamekuwa yakitekeleza tohara kinga kwa njia za kienyeji kutokana na mila,desturi na tamaduni zao hivyo ipo haja kwa wanaume kujitokeza kufanyiwa tohara iliyo salama. 

Katika hatua ya kudhibiti na kukabiliana na madhara hayo Shirika lisilo la kiserikali la IntraHealth International Inc linatekeleza mradi wa tohara katika mikoa saba inayopatikana kanda ya ziwa(Mwanza,Kagera,Mara,Simiyu,Shinyanga,Geita na Kigoma) ili kutoa huduma endelevu ya tohara pamoja na kuelimisha jamii kuthamini umuhimu wa kufanya tohara kinga iliyo salama,mradi ambao umewalenga watoto vijana wenye umri wa kuanzia miaka 10 na kuendelea. 

Mshauri wa huduma za tohara kutoka shirika la IntraHealth mkoa wa Geita,Dk. Peter Sewa amesema mradi huo unatekelezwa kuanzia mwaka 2018-2021 chini ya ufadhili wa PEPFAR kupitia CDC ikiwa ni miongoni mwa afua moja wapo za kujikinga na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,na unataraji kuwafikia zaidi ya wanaume laki nne. 

“Tuna huduma ambazo ni endelevu za kuwafikia wanaume ambao hawajafanyiwa tohara,tunafika kwenye maeneo yao hasa maeneo ambayo yanatajwa kuwa na idadi kubwa ya wanaume na hii itasaidia kuwalinda wanaume na hatari dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa pamoja na UKIMWI,na angalau tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huu mwitikio si haba kwani kwa siku tunapokea wanaume wasiopungua 10 kwenye vituo vilivyopo mkoani hapa,” alisema Sewa. 

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka mikoa saba ya utekelezaji wa mradi huo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita,Dk. Japhet Simeo amesema huduma ya tohara kinga iliyo salama itasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza maambukizi ya UKIMWI mkoani humo,na kubainisha mikakati ya mkoa kuwafanyia tohara watoto wachanga wenye umri wa mwezi sifuri hadi miezi miwili. 

“Kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI Mkoa wa Geita imepanda kutoka asilimia 4.7 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 5 mwaka 2017 hivyo Tohara ni afua ya muhimu sana,ukiachilia mbali matumizi ya kinga mfano mipira ya kondom mwanaume aliyefanyiwa tohara ana uwezo wa kukingwa kwa asilimia 60 japo tunasisitiza matumizi ya kujikinga,” alisema Dk. Simeo. 

Aidha waandishi wa habari kutoka mikoa saba inayopatikana Kanda ya Ziwa wameshirikishwa katika kufikia malengo ya mradi huo kwa kupatiwa elimu sahihi kuhusu huduma ya tohara kinga iliyo salama ambapo wametembelea maeneo mbalimbali kuona hali halisi ya utekelezaji wa mradi huo wa Tohara. Soma zaidi <<HAPA>>

Tazama picha hapa chini 
Waandishi wa habari wakichukua dondoo kutoka kwa muuguzi wa kituo cha afya Katoro Faustine Eduard huku nyuma kukiwa na kundi la watoto wakisubiri kufanyiwa tohara kinga salama. Picha zote na Malaki Philipo Malunde 1 blog
Baadhi ya wakazi wa mji wa Katoro wakisubiri kupata huduma ya tohara na wengine wakiwasubiri jamaa zao kufanyiwa tohara kinga iliyo salama.
Waandishi wa habari wakitekeleza majukumu kata ya Katoro wakati wamekwenda kuona hali halisi ya huduma za tohara katika eneo hilo.
Ofisi ya Afisa mtendaji wa kata ya Katoro,wilaya ya Geita,mkoani Geita.
Picha ya pamoja washiriki wa mafunzo ya tohara kinga kutoka mikoa saba ya Kanda ya Ziwa(Mwanza,Kagera,Mara,Simiyu,Kigoma,Shinyanga na Geita) mafunzo ya siku nne yaliyofanyika mkoa wa Geita.

Picha zote na Malaki Philipo Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم