Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JANGILI APEWA ADHABU YA KUANGALIA FILAMU JELA

Jangili mmoja nchini Marekani ameamriwa kuangalia filamu ya wanyama ya Bambi kila mwezi baada ya kukutwa na hatia ya kuua "mamia" ya mbawala.

Muwindaji huyo kutoka Missouri David Berry Jr anatakiwa kuangalia filamu hiyo walau mara moja kwa mwezi wakati akitumikia kifungo chake cha mwaka mmoja gerezani.

Alitiwa nguvuni mwezi Agosti pamoja na ndugu zake wawili kwa kuwaua mbawala, kisha kuwachinja na kuondoka na vichwa huku akiacha miili ya wanyama hao ioze, waendesha mashtaka wamesema.

Kesi hiyo ni moja ya kesi kubwa zaidi za ujangili kuwahi kuripotiwa kwenye historia ya jimbo la Missouri.

Pamoja adhabu ya kwenda jela kwa kuwinda mbawala kinyume cha sheria, Jaji Robert George alimuamuru Berry Jr "kuangalia filamu iliyoandaliwa na kampuni ya Walt Disney iitwayo Bambi, ambapo alitakiwa kuangalia kwa mara ya kwanza kabla ama Disemba 23 na baada ya hapo kuangalia walau mara moja kila mwezi," katika kipindi chote atachokaa jela.

Filamu hiyo ya katuni ya mwaka 1942 inaangazia maisha ya familia moja ya mbawara ambao walilazimika kuishi bila mama aliyeuawa na majangili. Waendesha mashtaka wanaamini jangili huyo ameua mamia ya mbawala pasi na kibali

Uchunguzi wa miezi uliofanyika kwenye majimbo kadhaa ulipelekea kunaswa kwa Berry Jr, baba yake David Berry Sr na kaka yake Kyle Berry, limeripoti gazeti la the Springfield News-Leader.

Japo idadi kamili ya mbawala waliouawa haijulikani, mhifadhi wa Kaunti ya Lawrence Andy Barnes amesema yaweza kufikia "mamia".

Berry Jr alipewa adhabu ya kwenda jela baada ya kukubali mashtaka yalikuwa yanamkabili.

Amepewa adhabu pia ya kwenda jela siku 120 kwa kukiuka masharti ya dhamana yake ya matumizi ya silaha za moto. Vibali vya jangili huyo na baba yake vya kuwinda vimefutwa moja kwa moja na Kamisheni ya Uhifadhi ya Missouri.
Chanzo : Bbc

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com