Na Andrew Chale, Bagamoyo
MWANAMUZIKI nguli wa miondoko ya Afro reggae, Jhikolabwino Manyika maarufu Jhikoman kwa kushirikiana na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Ijumaa ya 14 Desemba, 2018, amezindua rasmi albam yenye nyimbo sita tukio lililofanyika mjini Bagamoyo, Mkoani Pwani.
Jhikoman ambaye anatoka kwenye lebo ya AfriKabisa ameweza kuonesha ukongwe katika muziki huo kwa kufanya kazi pamoja na vijana wadogo ambao ni wanafunzi wa Chuo cha Sanaa TaSUBa na kukonga nyoyo mashabiki waliojitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi huo.
Albam hiyo ina beba nyimbo kama: Mara ya kwanza, Ndotoni, Safari, Bad mind,Time to love na Kuagana zilizo kwenye mtindo wa regge.
Katika uzinduzi huo, Msanii Vitalisi Maembe na wengine wakiwemo Sinaubi Zawose, Voice of Revolution, K’Gwana Shija pamoja na Bocka T waliwez kupamba jukwaa katika kusindikiza uzinduzi huo kwa kuimba nyimbo zao mbalimbali.
Jhikoman ameshukuru uongozi wa TaSUBa kwa ushirikiano wa kutayarisha albam na kuirekodi kupitia studio ya chuo hicho.
“Wasanii waliopiga vyombo na kuimba na mimi hapa jukwaani ndio nilioshirikiana nao katika albam hii ni wa TaSUBa. Nashukuru kwa Uongozi kuwapa fursa ya kufanya kazi hii. Lakini pia nawashukuru Watanzania kuendelea kutuunga mkoni katika kazi zetu na kwa sasa albam itakuwa inapatikana pale Afrikakabisa hapa Bagamoyo na maeneo mengine tutaendelea kuwatangazia” alieleza Jhikoman.
Na kuongeza albam hiyo imebeba ujumbe mbalimbali hivyo itakuwa inaburudisha na pia kufundisha Jamii.
“Hii ni hatua moja. Kwa sasa nimeanza na vijana hawa wanafunzi wa chuo cha Sanaa Bagamoyo. Muziki una ishi hivyo tunawarithisha vijana ili uendelee miaka na miaka kwa muda mrefu muziki wetu”, alieleza Jhikoman.
Aidha, Jhikoman amesema kwa sasa anatarajia kufanya ziara maalum kwa vyombo vya habari kwa lengo la kutangaza albam sambamba na kufanya shoo fupi katika vyuo na nyumba za tamaduni.
“Nimezindua albam ya safari ya gitaa baridi, lakini pia nimezindua na documentary yake ambayo yenyewe itaoneshwa sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye tamasha la Kimataifa la filamu za nchi za majahazi (ZIFF 2019), Kwenye tamasha la Sauti za Busara, (Busara Extra 2019).
Lakini pia nitafanya shoo fupi ya kuitangaza albam katika nyumba za tamaduni: Alliance francaise de dar es salaam na Goethe-Institut Tanzania zote za Dar es Salaam pamoja na Vyuo vikuu vikiwemo UDSM, Mkwawa na vingine vingi” alimalizia Jhikoman.
Safari ya Gitaa baridi ni Extended playlist (EP) ikiwa na maana albam yenye ujazo mdogo. Nyimbo zote sita ameandika mwenyewe huku lakini pia katika uimbaji ameimba mwenyewe kwa kushirikiana na wanafunzi hao wa TaSUBa.
Katika uzinduzi huo mashabiki walifurika kwa wingi katika ukumbi wa TaSUBa ambapo muda wote wakati wa mwanamuziki huyo akiwa jukwaani walilipuka kwa shangwe za mara kwa mara.
Naye Mtendaji Mkuu wa TaSUBa, Dkt. Herbert Makoye alieleza kuwa, Taasisi iliamua kushirikiana na Jhikoman kwa kuwa ni msanii mkubwa anayefanya kazi vizuri na kwa maadili, hivyo anaamini kwa kushirikiana naye wanafunzi wa TaSUBa watajifunza vitu vingi kutoka kwake ambavyo vitakuja kuwasaidia baada ya kuhitimu na kuanza shughuli zao za muziki hapo baadae.
Katika historia ya muziki, Jhikoman mbaye ni msanii maarufu wa muziki wa regge nchini, ndiye msanii wa kwanza kufanya wimbo na mwanamuziki Peetah Morgan wa kundi la Morgan heritage la nchini Marekani mnamo mwaka 2015, Morgan hertage ni nyota wa muziki wa raggie wanaoishi Marekani lakini asili yao ni Jamaica.
Wimbo wa Africa arise ndiyo uliowaunganisha Jhikoman na Peetah mogan, wimbo uliofanya vizuri katika anga za muziki duniani,kwa hiyo Jhikoman anaandika historia ya kuwa mwanamuziki wa kwanza Tanzania kushirikiana na mwanamuziki huyo wa Marekani, ambapo miaka miwili baadaye naye Diamond Platnumz alifuata nyayo za Jhikoman kwa kushirikisha Morgan hertage kwenye wimbo wake wa Hallelujah.
Social Plugin