Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema joto limeongezeka kutoka nyuzi joto 31 hadi 35 katika ukanda wa pwani kwenye mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Tanga na Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari leo Desemba 3, 2018 jijini Dar es salaam, Meneja wa Kituo Kikuu cha utabiri cha mamlaka hiyo, Samuel Mbuya amesema ongezeko la joto katika ukanda huo limetokana na mtawanyiko hafifu wa mvua za vuli na kuwepo kwa jua la utosi.
Mbuya amesema hali hiyo inatarajiwa kuisha Januari, 2019 lakini itarejea tena Februari, 2019 kwa sababu kutakuwa na jua la utosi.
"Joto limeongezeka kutokana na mwenendo wa kawaida wa jua la utosi na mtawanyiko hafifu wa mvua za vuli. Mvua zinaponyesha huwa zinapoza joto, tunatarajia hali hii itakwenda mpaka Januari," amesema Mbuya.
Watalaamu wa masuala ya afya wanasema joto linapoongezeka huchangia kudhoofisha nguvu ya mwili katika utendaji wa kazi, hususan pale mtu anapokuwa sehemu ya wazi, wanasema, mara kwa mara mtu anapaswa kunywa maji mengi ikiwa ni njia mojawapo ya kuboresha ufanisi wa mifumo katika mwili wa binadamu.
Chanzo - EATV