Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wa kikosi cha Chandarua cha mjini hapa, Sajenti Batisin Samda, kwa tuhuma za kuwaua kwa kuwapiga risasi watu wawili akiwamo mtalaka wake.
Askari huyo alitekeleza mauaji hayo akiwa kazini kwa kumuua askari mwenzake, Sajenti Juma Mkele na mtalaka wake, Veronica Kayombo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushy, jana alisema tukio lilitokea juzi majira ya saa 10 alasiri kwenye eneo la kambi hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda Mushy, inadaiwa kuwa Kayombo alikuwa amekwenda kwenye kambi hiyo kumpelekea hati ya wito kutoka idara ya ustawi wa jamii aliyekuwa mume wake, jambo ambalo linaonyesha lilisababisha askari huyo kupandwa na hasira.
Alisema siku hiyo ya tukio, Kayombo alipofika kwenye kambi hiyo, kabla ya kukutana na Samda, alionana na mkuu wake wa kazi na baadaye mkuu huyo alimpa maagizo Sajenti Mkele ili ampeleke kwake (Samda) akamkabidhi barua hiyo ya wito.
Kamanda Mushy alisema walipofika kwenye eneo alilokuwa anafanyia kazi mtuhumiwa huyo, ghafla wakiwa wanaendelea na mazungumzo kabla ya kumpa barua alipandwa hasira na kumfyatulia risasi Kayombo kisha kummalizia askari aliyekuwa ameongozana naye ambao walifariki dunia papo hapo.
Kamanda Mushy alisema polisi wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma dhidi yake.
Social Plugin