Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemsweka ndani Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule, Jimbo la Mwibara, wilayani Bunda, kwa kosa la kutafuna fedha za wanakijiji wilayani humo.
Waziri Lugola ambaye ni Mbunge wa jimbo hilo alitoa maamuzi hayo katika mkutano wa hadhara na wananchi hao uliofanyika kijijini hapo jana, baada ya kuwataka wananchi wenye malalamiko, maswali pamoja na ushauri watoke mbele ili aweze kuwasikiliza wananchi hao.
Baada ya agizo hilo, zaidi ya wananchi kumi walijitokeza na kuuliza maswali pamoja na kutoa kero zao, ndipo watu saba kati ya waliotoka mbele wakiwa wamepanga foleni walitoa tuhuma mbalimbali kuhusiana na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Wilbard Malea kutafuna fedha zikiwemo fedha za maendeleo ya kijiji pamoja na za faini kutokana na mashtaka yanayowasilishwa na wananchi kwake kwa ajili ya usuluhishi pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mkazi wa Kijiji hicho, Simon Joseph alimtuhumu katika mkutano huo, Mtendaji huyo alimfuata katika kikundi chao cha Muungano cha kuweka na kukopeshana alisema anaomba kukopa fedha shilingi 91,000 na kijiji kitarudisha fedha hizo, lakini mpaka leo hajazilipa na hakutumwa na Serikali ya Kijiji bali alisema uongo ili ajipatie kwa njia ya udanganyifu.
Pia Happyness Tabonwa mkazi wa kijiji hicho, alimlalamikia mtendaji huyo amechukua mbuzi wake watatu baada ya kushindwa kulipa shilingi 50,000, akaamua kuwakamata mbuzi hao na baada ya kumpeleka elfu 50 anayoidai Mtendaji huyo akashindwa kuwarudisha mbuzi hao kwa kuwa alishawauza na pesa kazitafuna.
Wananchi hao pia walimlalamikia Waziri Lugola, kuwa Mtendaji huyo wanapopeleka mashtaka yao, watuhumiwa hupigwa faini lakini fedha ikitolewa haiendi mfuko wa maendeleo ya kijiji bali fedha hizo uzitumia mtendaji huyo.
Pia mtendaji huyo analalamikiwa kuchukua simu ya mkononi ya Joseph Japhet ambaye alipohamia kijijini hapo aliambiwa alipe shilingi 50,000 ikiwa ni malipo kwa ajili ya maendeleo kijijini hapo, hata hivyo fedha hiyo hakuwa nazo ndipo Mtendaji huyo akamnyang’anya simu yake.
Wakati wananchi hao wanatoa malalamiko hayo, mtendaji huyo alikuwa mbele katika mkutano huo baada ya kuitwa na Waziri Lugola ili aweze kujibu tuhuma hizo zikiwemo za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyi pamoja na kuwadhulumu wananchi mbalimbali wa kijiji hicho.
Akijibu tuhuma hizo Mtendaji huyo, Malea alizikana tuhuma hizo na baada ya kubanwa huku wananchi hao wakielezea kwa mifano, ndipo akakiri kutafuta fedha za wananchi hao na akaahidi katika mkutano huo atawalipa wananchi wote wanaomdai.
Baada ya kukiri ndipo Waziri Lugola akamwita Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara Wilayani Bunda, Mkaguzi Boniface Mwalupale, ili Polisi walipo katika mkutanon huo wamkamate Mtendaji huyo na akafunguliwe mashtaka endapo atashindwa kuwalipa wananchi mbalimbali wanao mdai kama alivyokiri.
“Ndugu wananchi, kwanini hawa viongozi mnaowachagua wanakua sio waadilifu?, nimefanya mikutano katika vijiji mbalimbali nimekutana na changamoto kama hii, na pia katika kijiji ambacho tumetoka, Mtendaji wa Kijiji pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji hicho wametafuna fedha za mchanga zilizotolewa na kampuni inayojenga barabara ya Bunda hadi Kisorya, tunaenda wapi ndugu zangu, viongozi wadokozi kama hawa lazima tuwakamate, najua polisi mnahamu ya kukamata mhalifu, mkamateni ili akaeleze hizo fedha alizipeleka wapi na kwanini alizitafuna fedha za wanakijiji,” alisema Lugola.
Akizungumza saa mbili baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara (OCS), Mwalupale alisema Mtendaji huyo anadaiwa zaidi ya shilingi 300,000 lakini mpaka sasa ameshatoa 206,000, hata hivyo hawajamuachia bado yupo polisi mpaka atakapomaliza kulipa madeni yote.
“Bado hatujamtoa mtuhumiwa huyo ambaye amejipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utapeli, mpaka sasa tayari ametoa 206,000, bado mbuzi watatu hajalipa,” alisema OCS Mwalupale.
Lugola anaendelea na ziara yake kwa kutembelea vijiji vyote jimboni kwake Mwibara akisikiliza kero za wananchi pamoja na kuhamasisha kilimo cha mazao ya pamba, mahindi, mpunga, viazi na mengineyo ambayo wakazi wa jimbo lake wanalima mazao hayo kwa wingi.