Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU WA CCM AMWAGIZA WAZIRI KUTAFUTA FEDHA KUWALIPA WAKULIMA WA KAHAWA


Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amemwagiza Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa kutafuta fedha za kuwalipa wakulima wa zao la kahawa mkoani Kagera kwa bei inayoridhisha kulingana na gharama watumiazo katika uzalishaji.

Dk Bashiru alitoa agizo hilo juzi mbele ya wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa huo wanaotoka wilaya za Ngara Kyerwa na Karagwe alipokutana nao mjini hapa.

Katibu mkuu huyo wa CCM alitoa agizo kwa Bashungwa ambaye ni Mbunge wa Karagwe (CCM) aliyekuwapo kwenye

kikao hicho kwenda kuhakikisha bei inaboreshwa ili kuwavutia wakulima wa zao hilo.

Alisema licha ya Serikali kuzuia magendo ya kahawa kutoka Kagera kuingia Uganda lakini inanunuliwa kwa kificho kisha inasafirishwa na kuwekwa katika kasha au kopo la robo kilo hadi nje ya nchi ikiwa na thamani kubwa hasa China.

“Waganda wananunua kahawa kwa magendo wanaikaanga na kuifunga kwa kuweka picha ya mwanamke mrembo wa Kiganda, wanaisafirisha hadi China kupitia bandari yetu inauzwa kakopo Sh40,000 iweje mkulima apatiwe Sh1,000?” alihoji Dk Bashiru.

Pia alimuagiza Mkurugenzi Halmashauri ya Ngara, Aidan Bahama kutowanyang’anya wananchi ardhi kwa madai ya kuwagawia wawekezaji kutoka Korea Kusini.

“Nilikupigia simu kukuzuia sasa nakupa ‘live’ sitaki kusikia wawekezaji wa nje wanapewa ardhi bila kufuata utaratibu wa kuridhiwa kwanza na mkutano mkuu wa vijiji,” alisema.

Mkuu Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali, Marco Gaguti alisema katika kupambana na biashara ya magendo ya kahawa wilaya ya Misenyi imekamata magari 12 yenye tani zaidi ya 60 na pikipiki zilizokuwa zikisafirisha Uganda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com