WANAFUNZI 12,399 WACHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA 2019 SIMIYU



Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju akitoa taarifa ya hali ya ufaulu katika Mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka 2018, katika kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2019 kilichofanyika Desemba 14, 2018 Mjini Bariadi.



Na Stella Kalinga, Simiyu

Jumla ya Wanafunzi 12,399 mkoani Simiyu wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2019 katika shule za Serikali za kutwa na bweni kwa awamu ya kwanza.

Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini Desemba 14, 2019 wakati akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa Kidato cha kwanza kwa mwaka 2019 Mjini Bariadi.

Sagini amesema jumla ya wanafunzi waliofaulu Mtihani wa Darasa la Saba ni 24,983 sawa na asilimia70.68 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani, ambapo amebainisha kuwa wanafunzi 12, 584 kati ya 24,983 waliofaulu hawajachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa miundombinu ya elimu.

Sagini amesema lengo la Serikalini kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanaenda sekondari hivyo, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani Simiyu kuhakikisha kuwa wanafanya jitihada katika ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu, ili wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba waweze kuanza kidato cha kwanza kwa wakati.

"Lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata nafasi ya kujiunga kidato cha kwanza ; nimetoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kukamilisha miundombinu inayohitajika ili wanafunzi watakaochaguliwa awamu ya pili waweze kuripoti shuleni kabla ya Februari 15, 2019"

"Nawasihi wazazi na walezi wa wanafunzi watakaokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa awamu ya kwanza kuwa wavumilivu wakati Halmashauri zinajiandaa kuwapokea wanafunzi hao" alisema Sagini.

Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju amesema ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 67.73 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 70.68, ambapo wavulana wameonekana kufanya vizuri zaidi kwa ufualu wa asilimia 74.61 na wasichana asilimia 67.57.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Bahame Kaliwa amesema mahitaji ya miundombinu yameongezeka kutokana na ufaulu kuongezeka kila mwaka, hivyo jitihada zitafanyika ili kuhakikisha miundombinu inayohitajika inajengwa na wanafunzi wenye sifa za kwenda kidato cha kwanza wanapata nafasi.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Chenge, Mwl.Mhinga Bulenzi amesema wamefanya mikutano kadhaa na wazazi na wakakubali kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya elimu ili wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba na hawakuchaguliwa kwa awamu ya kwanza waanze kidato cha kwanza ifikapo Februari 15, 2019.

Jumla ya wanafunzi 35,346 kati yao wasichana wakiwa 19,743 na wavulana 15,603 walifanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu 2018 mkoani Simiyu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم