Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kata ya Okaoni amejikuta akilala rumande kwa saa 48 kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya baada ya kiongozi huyo kulalamikiwa na wananchi, kuwa amemiliki shamba kwa muda mrefu bila kuliendeleza.
Diwani huyo ambaye anafahamika kwa jina la Moria Makoi alituhumiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya kuwa kupitia baraza la madiwani alimilikishwa shamba la kahawa Nkwasira lenye ukubwa ekari 500.
Akizungumza mbele ya Mkutano huo, Dc Sabaya amesema "sina kumbukumbu na mwekezaji, huyu ambaye pia ni diwani wa CCM, haiwezekani shamba hili alilopewa na serikali akalime maharage badala ya kulima kahawa."
Hali ya kukamatwa kwa viongozi kwa upande CCM imekuwa mara chache kutokea kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho, lakini imekuwa ni tukio la mara kwa mara kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ambao mara kwa mara wamekuwa wakituhumiwa kuvunja sheria.
Machi 2018 Mbunge wa Jimbo la Hanang, mkoani Manyara Dkt Mary Nagu (CCM) na Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo walishikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo kwa amri ya Mkuu wa wilaya.
Chanzo: Eatv