Mkimbiaji wa mbio ndefu kutoka Kenya Eliud Kipchoge ndiye mwanariadha bora wa kiume kwa mwaka 2018.
Kipchoge ametawazwa wadhifa huo mkubwa katika ulimwengu wa michezo katika hafla iliyoandaliwa na shirikisho la riadha duniani, IAAF, usiku wa Jumanne huko Monte Carlo, Monaco.
Tuzo hiyo inathibitisha kuwa Kipchoge mwenye miaka 33 ndiye mkimbiaji mbio za masafa marefu bora zaidi wa zama hizi.
Septemba mwaka huu, Kipchoge aliandika rekodi mpya ya mbio za 2018 Berlin Marathon, kwa kukimbia kilomita 42 kwa muda wa saa 2 dakika 1 na sekunde 39, na kuvunja rekodi ya mwenzake wa Kenya Dennis Kimetto aliyeweka rekodi mpya ya dunia ya saa 2, dakika 2 na sekunde 57 aliyokimbia mwaka wa 2014 katika mbio hizo. Hii ilikua ni mara ya tatu kwa Kipchoge kuibuka mshindi kwenye mbio hizo za Berlin marathon.
Kipchoge pia alishinda medali ya dhahabu mwaka 2016 katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika jijini Rio de Janeiro, Brazil.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameongoza mamia ya Wakenya ambao wametuma ssalamu zao za pongezi kwa Kipchoge baada ya kutuzwa.
Katika salamu zake alizozituma kupitia ukurasa wake wa Twitter, Kenyatta amesema 'utawala' wa Kipchoge kwenye riadha umemfanya bingwa huyo kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu na pia kuhakikisha kuwa Kenya inaendelea kuwa kinara wa riadha duniani.
Chanzo:Bbc
Social Plugin