Kutokana na kina cha bahari ya Hindi katika eneo la Mnazi Bay Msimbati mkoani Mtwara kuendelea kumomonyoka siku hadi siku kuelekea nchi kavu, huenda nchi ikajikuta gizani kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
Hayo yamesemwa jana Jumatatu Desemba 4, 2018 na Naibu mkurugenzi wa Kampuni ya Maurel & Prom Tanzania inayohusika na kuchimba gesi, Elias Kilembe kwa Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alipotembelea visima hivyo vya gesi.
Kilembe alisema siku hadi siku bahari inasogea nchi kavu kuelekea kilipo moja ya kisima cha gesi na mitambo hali inayowapa wasiwasi.
“Hata mwaka jana ulitokea mmomonyoko lakini haukuwa tishio kama wa mwaka 2015, lakini ukija hapa baharini unakuta mchanga umeondoka wote na kupotea, kweli ni tishio kwa kambi hii,” alisema Kilembe.
Waziri wa nishati, Dk Kalemani amesema hali halisi inaonekana na hakuna haja ya utafiti, bali kinachotakiwa kufanyika ni kujengwa kwa ukuta haraka ambao utatenganisha kisima kilipo na bahari ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
“Kuanzia sasa anzeni kufanya utaratibu wa kujenga ukuta kwa sababu mtafika mahala mtakosa hata pa kuweka ukuta maji yakishafika huku, ni vizuri kuanza sasa ili msije kukumbwa na dhoruba kubwa, haya ni maagizo ya haraka haraka wala si jambo la kufanya utafiti,” amesema Dk Kalemani.