Shirika lisilo la Kiserikali KIWOHEDE ambalo linatekeleza mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa vijana wilayani Kahama Kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Sida la nchini Sweden, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Serikali, wameadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wilayani humo, na kuitaka jamii iondokane na vitendo hivyo.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Desemba 10,2018 kwenye Uwanja wa Nje wa Bwalo la Polisi wilayani Kahama, kwa kutanguliwa na maandamano yalioanzia katikati ya Mji wa Kahama,kwa kuonyeshwa mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.
Awali Mratibu wa Mradi wa Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Kiwohede wilayani Kahama Amos Juma, ambao wanapinga mimba na ndoa za utotoni, aliitaka jamii kuachana na tabia ya kung’ang’ania kuenzi mila na desturi ambazo zimeshapitwa na wakati ikiwa ndiyo chanzo kikubwa cha kuendelea kutokea matukio ya ukatili wa kijinsia.
“Mila na desturi kandamizi zimekuwa kichocheo kikubwa cha matukio ya kikatili ikiwemo mimba na ndoa za utotoni,hivyo ni lazima wadau tushirikiane kuhakikisha tunaondoa mila hizi ambazo zimekuwa zikikatisha ndoto za watoto wetu,”,alisema Juma.
Akizungumza katika maadhimisho hayo mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha, aliitaka jamii kuondokana na vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo, ikiwamo na ongezeko la wajane, watoto wa mitaani, ubakaji, mimba pamoja na ndoa za utotoni.
Alisema ili kukomesha matukio hayo ya ukatili wa kijinsia inapaswa watu wote kushirikiana na kuwa wamoja kukataa vitendo hivyo, pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale ambao bado wanaendeleza ukatili, hali ambayo itasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza ama kumaliza kabisa matukio ya ukatili ndani ya jamii.
“Natoa wito kwa wananchi tushirikiane kabisa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, na wale ambao wanafanyiwa matukio mabaya watoe taarifa katika mamlaka zinazohusika, kama mama Fatuma Mabanga ambaye alibakwa na kisha kutobolewa macho ambapo mtuhumiwa alikatwa na kisha kufungwa jela,”alisema Macha.
“Nawasihi pia wazazi mtekeleze majukumu yenu kwa watoto wenu, muache tabia ya kuwatelekeza ikiwamo kuwasomesha, kutowatimizia mahitaji yao, na kuacha tabia ya kuwachungisha mifugo pamoja na kuwaozesha ndoa za utoto kwa tamaa ya kupata mali na hatimaye kuzima ndoto zao”,aliongeza.
Pia alipiga marufuku kwa watu ambao wamekuwa na tabia ya kusafirisha watoto wadogo kwa kuwarubuni wanakwenda kuwasomesha, na matokeo yake huanza kuwatumikisha kazi za ndani, mashambani kwenye baa, migodini na kwenye majumba ya madanguro kuwa atakaye bainika atashughulikiwa kisheria.
Naye kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama Mji Robert Kwema, ametaja takwimu za vitendo vya ukatili wa kijinsia kuanzia kipindi cha Januari hadi Novemba 2018 kuwa jumla ya matukio 1,341 yameripotiwa, ukiwamo ukatili wa Kingono matukio 76, kimwili 140, kihisia 133,kiuchumi 118, kutelekezwa 26.
Pia alitaja takwimu za mimba za utotoni 26 na ndoa 26 pamoja na ajira kwa watoto 77, huku akitoa wito kwa wazazi na watoto kuacha tabia ya kutotoa ushirikiano mahakamani pale kesi zinapofunguliwa, ili watuhumiwa wapate kuchukuliwa hatua kali za kisheria na kuweza kukomesha vitendo hivyo.
Naye mmoja wa waathirika wa matukio hayo ya ukatili wa kijinsia Fatuma Mabanga (50) mkazi wa Kahama mwenye watoto 13, ambaye alibakwa vichakani na kisha kutobolewa macho mwaka 2014, ambapo alitelekezwa na mumewe Vicent Nkwabi, aliiomba mahakama iwe inatoa hukumu haraka kwa watu wanaotenda matukio ya kikatili ili wafungwe jela na siyo kuzichezea kesi hizo.
TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Mtandao wa Polisi wanawake wilayani Kahama wakiongoza maandamano huku wakishika mabango yenye ujumbe mbalimbali kwa ajili ya kutoa ujumbe kwa jamii kuacha vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mabinti wanufaika wa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama wakiwa kwenye maandamano na kuonyesha mabango yenye ujumbe wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.
Maandamano yakiendelea katikati ya mji wa Kahama kuelekea kwenye uwanja wa bwalo la Polisi na kutolewa ujumbe mbalimbali za kupinga ukatili wa kijinsia kwa jinsi zote.
Mabinti wanufaika wa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama wakiwa kwenye maandamano na kuonyesha mabango yenye ujumbe wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.
Maandamano yakiendelea.
Mtandao wa Polisi wanawake ukiongoza maanadamano katika maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Ujumbe mbalimbali ukisomeka katika mabango juu ya kupinga ukatili wa kijinsia wilayani Kahama.
Mabinti wanufaika wa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka katika Shirika la KIWOHDE wilayani Kahama, wakiwa kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Mabinti wanufaika wa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka katika Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama, wakiwa kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wakionyesha ujumbe wa kupinga ukatili huo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na kuitaka jamii iondokane na vitendo hivyo ili wananchi wa jinsia zote wabaki kuwa salama, pamoja na watoto kutimiza ndoto zao.
Awali Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Kahama Sophia Jongo akifungua maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wilayani humo.
Mratibu wa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama Amos Juma akielezea namna changamoto ambazo wanakutana nazo katika kutekeleza mradi wao huo,ambao unapinga matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo mimba na ndoa za utotoni, kuwa kiwazo kikubwa ni jamii kuendekeza mila na desturi potofu ambazo zimeshapitwa na wakati, na kuitaka iachane nazo.
Victoria Athony ambaye ni binti mnufaika na mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama,akiwataka wazazi kuacha tabia ya kunyanyasa watoto wao pamoja na kutowabagua watoto wa kike ikiwemo kuwapatia elimu, ambapo baadhi yao huamua kutoroka makwao na kwenda kujitegemea na mwisho wa siku wanaambulia ujauzito.
Mohamed Mgalula ni kijana mnufaika na mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama, anaelezea namna maadhimisho hayo ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia kuwa ni muhimu kwao vijana katika kuhakikisha wanapaza sauti kwa mamlaka husika ili kuwashughulikia watu ambao bado wanaendekeza vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.
Kaimu mkurugenzi wa Kahama Mji Robert Kwema akitaja takwimu za ukatili wa kijinsia kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu, kuwa jumla ya taarifa za ukatili zimewasilishwa 1,341 huku utelekezaji watoto ukiongoza matukio 362.
Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kahama Richard Kayula, akitoa elimu kwenye maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wilayani humo, na kukemea kuendekeza vitendo vya rushwa ambavyo ni moja ya vichocheo vya kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia, zikiwamo Rushwa za ngono, pamoja na watuhumiwa kuhonga na hatimaye kesi kuisha bila ya kufungwa jela.
Fatuma Mabanga(50) ambaye ni mkazi wa wilaya ya Kahama mwenye watoto 13 akielezea namna alivyofanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kubakwa mwaka 2014 na kisha kutobolewa macho na mhusika na baada ya tukio hilo mumewe Vicent Nkwabi alimkimbia na kumuachia watoto hao kuwalea mwenyewe huku yeye akienda kuoa mwanamke mwingine.
Mkuu wa dawati la jinsia wilayani Kahama Zainabu Mangalla akielezea namna jeshi hilo linavyomsaidia mama huyo ikiwemo kumpatia huduma za chakula na malazi, ikiwa watoto wake hawana uwezo ambapo hufanya biashara ndogondogo ikiwemo kuuza mbogamboga.
Kaimu mkurugenzi wa Kahama Mji Robert Kwema akielezea namna serikali inavyomsaidia mama huyo kwa kushirikiana na wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia ambapo kikundi cha akina mama wajasiriamali wamemfungulia akaunti ya NMB ili msaada wa fedha anazozipata zituzwe benki.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akimkabidhi kadi ya benki ya NMB Fatuma Mabanga pamoja na pesa taslimu zilizochangwa na wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia shilingi 96,8500.
Afisa Ardhi wa halmashauri ya Kahama Mji Radislaus Masumbuko akitoa msaada wa kiwanja kwa mama huyo Fatuma Mabanga kwa ajili ya kujengewa nyumba ya kuishi.
Mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe wilayani Kahama Neema Sawaka naye akiunga mkono kwa kutoa msaada wa Bati Tano kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba ya mhanga huyo wa ukatili wa kijinsia Fatuma Mabanga, huku akishikana mkono wa pongezi na mkuu wa kituo cha Polisi wilayani Kahama Sophia Jongo, akifuatiwa na mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha.
Wanafunzi kutoka shule ya msingi Kahama "B" wakiimba Ngonjela yenye ujumbe wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Vijana kutoka kundi la Mwanakwela wakitoa burudani kwenye maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Wafanyakazi wa halmashauri ya Kahama Mji wakiwa na askari Polisi wakivuta Kamba kupimana nguvu,ambapo kundi la wafanyakazi ndiyo liliibuka na ushindi huo.
Mwanakwela akiendelea kutoa burudani kwenye maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuchezea baiskeli.
Mtandao wa Polisi wanawake wilayani Kahama wakitoa burudani kwa kucheza kwaito kwenye maadhimisho hayo ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Mwenyekiti wa mtandao wa polisi wanawake wilayani Kahama Sophia Jongo akielezea zawadi ambazo wanazitoa kwa watoto wanaolelewa kwenye vituo vya watoto yatima katika kituo cha Mvuna pamoja na Peace cha Nyahanga,kwa kutao zawadi za sabauni za unga mifuko miwili, sabani kiche box 2, mafuta ya kupikia ndoo mbili, Sukari mifuko miwili, unga mifuko 4, zikiwamo na taulo za kike.
Mwanakwela akiendelea kutoa burudani kwenye maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuchezea baiskeli.
Baadhi wa waandishi wa habari wilayani Kahama wakichukua matukio mbalimbali kwenye siku hiyo ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia.
Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog.