Inaelezwa kuwa kocha wa klabu ya Tottenham Hortspurs, Mauricio Pochettino amewaeleza wachezaji wake kuwa hafurahishwi na kitendo cha wachezaji kupiga picha za 'Selfie' katika vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa hawajashinda kombe lolote.
Kocha huyo ameonesha kutofurahishwa na kitendo cha wachezaji wa Arsenal kupiga Selfie katika vyumba vya kubadilisha nguo, wakifurahia ushindi walioupata dhidi ya Spurs wa mabao 4-2 katika uwanja wa Emirates wikiendi iliyopita.
"Ni sahihi kushangilia pale unaposhinda ubingwa, kama ambavyo mimi nilifanya nilipokuwa mchezaji. Nakubali kuwa kuwaonesha mashabiki furaha yako ni kitu muhimu lakini ni vizuri pale unaposhinda kombe," amesema Pochettino.
"Ninakubali kuwa watu wanahitaji hicho, kwasababu ndivyo ulimwengu mpya ulivyo lakini mimi ni mtu wa kizazi cha zamani kwahiyo sipendi vitu hivyo," ameongeza.
Pochettino mwenye umri wa miaka 46, alishinda ubingwa wa Copa del Rey kama mlinzi wa klabu ya Espanyol.
Pia kocha huyo amezungumzia mchezo wa EPL leo usiku dhidi ya Southampton, utakaopigwa katika uwanja wa Wembley, ambapo amesema, "ninakwenda na vijana wangu kama vile mbwa wanavyokwenda msituni, ambapo matarajio yetu sio kufurahia na mpinzani bali ni kufurahia na mashabiki wetu".
Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Arsenal, sasa Spurs inakamata nafasi ya tano ya msimamo wa EPL ikiwa na alama 30 sawa na Arsenal iliyopo nafasi ya nne kutokana na kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.