Madaktari nchini Zimbabwe wamelazimika kuvaa kondomu mikononi badala ya mipira ya mikono (gloves) walipokuwa wakimhudumia mgonjwa, kutokana na ukosefu wa kifaa tiba hicho.
Madaktari hao ambao ni wanachama wa 'Zimbabwe Hospital Doctors Association'(ZHA), wameamua kuanzisha mgomo wakitaka kuboreshwa kwa mazingira yao ya kazi, sambamba na kutaka mshahara wao ulipwe kwa dola za Kimarekani.
Mmoja wa madaktari hao, Prince Butawo alisikika akimwambia mwandishi wa habari nchini Zimbabwe kuwa wanalamika kutumia condom wakati wa uchunguzi wao, kutokana na uchache wa gloves.
“Tuna process zingine ambazo tunazifanya unatakiwa uvae mipira, lakini hatuna hivyo tunalazimika kutumia condom, kwa mfano kwa watu wa masuala ya wanawake, badala ya kutumia mikono mitupu, tunalazimika kuvaa condom mikononi kujilinda, hata mtu akija ana matatizo ya kibofu tunalazimika kumwambia akanunue mfuko wa kuwekea mkojo, kwani hospitali hakuna”, amesema Butawo.
Naye Katibu Mkuu wa ZHDA, Mthabisi Bhebhe, amesema kwamba walishapeleka malalamiko yao mengi zaidi ya hayo kwa Waziri wa Afya, lakini mpaka sasa hawajafikia muafaka wa kuyatatua, hivyo wamekataa kusitisha mgomo wao mpaka pale yatakapotatuliwa.