Serikali imefunga kwa muda akaunti 191 za benki zinazomilikiwa na wakulima wa korosho kupisha uhakiki wa kina wa umiliki wa korosho walizouza.
Uamuzi huo unakuja wakati ikiwa imeshaingiza Sh3.8 bilioni kwenye akaunti hizo katika mfululizo wa uhakiki na ulipaji wakulima wa zao hilo unaoendelea nchini.
Akizungunza na gazeti la The Citizen, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema wakulima wenye akaunti hizo wameuza zaidi ya kilo 1,500 kwenye vyama tofauti vya msingi, hivyo ni lazima umiliki wa korosho walizouza uhakikiwe.
“Hatua hii ni muhimu (ya kufunga akaunti hizi kwa muda) ili kupisha uhakiki kwa sababu utaratibu unataka mkulima aliyeuza zaidi ya kilo 1,500 za korosho aonyeshe shamba lake lilipo kwa timu yetu ya uhakiki,” alisema Hasunga.
“Lakini uchunguzi wa awali umeonyesha kuna baadhi ya wakulima wameuza kiasi kinachofikia kilo 3,000 za korosho kwenye vyama vya msingi tofauti.”
Hata hivyo, waziri huyo alisema Serikali bado haijapata kiasi halisi cha korosho ambacho wamiliki wake wameshindwa kuonyesha mashamba yao, lakini alisisitiza kuwa tatizo hilo bado ni kubwa.
Akizungumzia uhakiki na malipo kwa wakulima, alisema tayari Sh206.092 bilioni zimeshalipwa kufikia Disemba 27 kati ya hizo, Sh188.378 bilioni zilikuwa zimewafikia wakulima kabla ya sikukuu ya Krismasi.
“Wakulima 100,534 wameshalipwa bila kujali ni mara ngapi walipeleka korosho kwenye chama cha ushirika cha msingi. Wakulima hawa wanatoka katika vyama vya msingi 398 kati ya vyama 617 vilivyosajiliwa nchini na vyama 504 vinavyopatikana katika mikoa mitatu ya Mtwara, Lindi na Ruvuma,” alisema.
Alisema tani 188,799. 4 za zao hilo zimeshakusanywa katika maghala mbalimbali na kwamba tani 30,226.25 zimehamishiwa kwenye maghala mengine ili kutengeneza nafasi korosho zilizo mikononi mwa wakulima kupokewa.
Takwimu za Serikali zinamaanisha kuwa Sh206.092 bilioni zilizotolewa ni malipo kwa tani 62,452.333 kati ya tani 188,799 zilizokusanywa na tani 126, 347.07 zinasubiri mchakato wa malipo.
“Mchakato hautakamilika mwisho wa mwezi huu kama tulivyotarajia kutokana na changamoto zilizojitokeza, matumaini yetu ni kwamba uhakiki na malipo yatakamilika mwishoni mwa mwezi Januari mwakani.”
Chanzo :Mwananchi
Social Plugin