Watu wanne wamefariki dunia mkoani Kagera katika kusherehekea sikukuu za Krismasi na siku ya Boxing Day , kufuatia matukio manne yaliyotokea kwa nyakati tofauti mkoani humo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Revocatus Malimi, lipo tukio la Desemba 25 katika kijiji cha Kigorogoro wilaya ya Kyerwa, mwanamke alipigwa na mpenzi wake wakati wakisherehekea sikukuu hiyo kwenye moja ya majumba ya starehe, ambapo mwanaume huyo alimtuhumu mpenzi wake kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine.
Katika tukio la pili Kamanda huyo amesema kuwa Justus Clemence mwenye umri wa miaka 42 mkazi wa kitongoji cha Itokozi wilayani Biharamulo anayedaiwa kuwa na ugonjwa wa akili, alipoteza maisha baada ya kupigwa na watu waliomtuhumu kuiba kondoo wa mwanakijiji mwenzao.
Aidha kamanda huyo amesema kuwa bibi aliyetambuliwa kwa jina la Magdalena Martine mwenye umri wa miaka 75 amefariki Desemba 25 mwaka huu saa tisa mchana katika kijiji cha Migara Bukoba vijjini, baada ya kulipukiwa na moto wakati akipika katika jiko lake lililoezekwa kwa nyasi na kuwa alifariki kutokana na moto kumzidi nguvu.
Pia kamanda Malimi amezungumzia tukio jingine la Ronald Hitiman raia wa Rwanda ambaye amepoteza maisha Desemba 26 baada ya kujinyonga katika chumba chake alimokuwa akiishi katika mtaa wa Kamizilente kata Rwamishenye katika manispaa ya Bukoba.
Chanzo - EATV
Social Plugin