Baba mlezi, Mmanga Mrope (47), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tunduru kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa miaka minane.
Akisomewa mashtaka juzi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Abdalah Amwero, mwendesha mashtaka Inspekta Steven Msongaleli alidai kuwa kwa mara ya mwisho mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Desemba 6, mwaka huu, majira ya saa 4.40 usiku baada ya kumvamia na kumziba mdomo mtoto huyo na kufanikisha azima hiyo.
Msongaleli alidai kuwa mtuhumiwa huyo alianza tabia ya kumwingilia mtoto huyo anayesoma darasa la tatu (jina la shule linahifadhiwa) pamoja na kumfanya kinyume cha maumbile katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Alisema kwa kufanya hivyo Mrope alifanya kosa kinyume cha sheria namba 130 (1) na (2c) vya sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16 kama ilivyofanyiwa mabadiliko mwaka 2002.
Aidha, alidai kuwa mtuhumiwa huyo alibainika baada ya mtoto huyo kumwambia mwalimu wa darasa lake baada ya kumhoji kutokana na mtoto huyo kukosa furaha wakati wote anapokuwa shuleni.
Ilidaiwa kuwa baada ya kubaini hivyo, walimu walimwita mtoto huyo na kuzungumza naye kirefu na kuwaeleza kuwa mtuhumiwa alikuwa akimtishia kumuua na kukimbilia nchi jirani ya Msumbiji endapo angetoasiri hiyo.
Kutokana na taarifa hiyo, ilidaiwa kuwa mtoto huyo alipelekwa katika hospitali ya wilaya ya Tunduru kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na vipomo kuthibitisha kufanyiwa kitendo hicho.
Mwendesha mashtaka alidai kuwa baada ya vipimo kubaini hivyo, mtuhumiwa alikamatwa ili kupisha sheria kufuata mkondo wake.
Mtuhumiwa huyo alikana kufanya kosa hilo na kupelekwa rumande baada ya kukosa wadhamini.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi keshokutwa kwa ajili ya kusikilizwa na kwamba upelelezi umekamilika.