Mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Wilunze mwenye umri wa miaka 14 anatuhumiwa kuwalawiti wanafunzi wenzake ambapo katika tukio la hivi karibuni alimlawiti mtoto wa miaka mitatu.
Hayo yalibainishwa na Mtendaji wa Kijiji Cha Wilunze Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Georgina Richard wakati akizungumza juzi katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa vijiji na kata kupitia mradi wa kutokomeza ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni unaotekelezwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Woman Wake Up (WOWAP).
Alieleza kuwa tukio la kulawitiwa mtoto wa kiume wa miaka mitatu lilitokea Novemba 26, mwaka huu kijijini hapo. Alisema mtuhumiwa huyo ni mtoro wa kudumu na mara ya mwisho alikuwa akisoma darasa la tatu Shule ya Msingi Wilunze.
Alisema siku ya tukio mtuhumiwa huyo alimuingiza mtoto huyo kwenye nyumba ambayo haijamalizika na kumfanyia kitendo hicho.
“Aliyeshuhudia kitendo hicho ndio alikwenda kutoa taarifa kwa mama wa mtoto ambapo mtoto huyo mdogo alipekekwa hospitali kupimwa na kukutwa na manii mapajani ambazo zimekauka, na alikuwa ameingiliwa kinyume na maumbile,” alisema.
Alisema ndipo mama huyo alipewa barua na kwenda kuripoti tukio katika kituo cha Polisi Chamwino. Mtendaji huyo wa Kijiji alisema mtuhumiwa huyo bado hajulikani alipo na kesi hiyo iko kwenye upelelezi.
“Hali ya mtoto inaendelea vizuri, tukapata taarifa kuwa mama mtuhumiwa alimfuata mama wa mtoto aliyelawitiwa ili waweze kuelewana nikawaambia sitaki kusikia kitu kama hicho wasubiri sheria ifuate mkondo wake,” alisema.
Alisema kutokana na uchunguzi aliofanya baada ya tukio hilo ikabainika kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akiwalawiti baadhi ya watoto wa darasa la kwanza na la pili.
“Tulikwenda hadi shuleni tukawabaini watoto waliofanyiwa kitendo hicho wako wa kike na wengine wa kiume, tukagundua watoto walikuwa wakifanyiwa vitendo hivyo lakini walikuwa hawasemi,” alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo mara kadhaa amekuwa akifikishwa ofisi ya Kijiji kutokana na utoro na mpaka sasa anaendelea kutafutwa ili sheria ichukue mkondo wake.
Chanzo : Habarileo
Social Plugin