TAKUKURU YAELEZA ILIVYOKUTA BAHASHA YA KAKI MEZANI KWA WAZIRI LUKUVI


Na Karama Kenyunko, Blogu ya Jamii

KAIMU Kamishna Msaidizi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi Wilson Luge (39) ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kuwa fedha alizoenda kuhakiki katika ofisi ya Waziri wa Ardhi zinazodaiwa kutolewa kama rushwa kwa Waziri William Lukuvi zilikuwa zimehifadhiwa katika mfuko wa kaki.

Luge ameyasema hayo leo Desemba 11, 2018 wakati anajibu swali la Wakili wa utetezi Imani Madega dhidi ya kesi ya tuhuma za rushwa ya Sh. Milioni 90 kwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group Co.ltd na Kiluwa Free Processing Zone,Mohamed Kiluwa alipokuwa akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Samwel Obasi.

Amedai mahakamani hapo kuwa Julai 16 mwaka huu akiwa kazini kati ya saa saba mchana hadi saa 10 jioni, walikuwa wanaangalia mfumo wa kielekroniki wanaoutumia kama unafanya kazi vizuri, Esquires na Kamishna Mkuu wa Ardhi Mary Makondo na kuwaelekeza waende ofisi ya Waziri Lukuvi.

Pia amedai walipoingia walikuta watu mbalimbali huku mezani kukiwa na mfuko wa kaki uliokuwa umefungwa ambao hakujua ndani yake kulikuwa na nini na kwamba mfuko huo ulifunguliwa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru na kutoa fedha ambazo ni mabunda manne ya Dola za Marekani 40,000 ambapo waliwataka yeye na Hellen Philipo walihakiki fedha hizo.

Mapema akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Takukuru Maghela Ndimbo, shahidi huyo wa sita amedai Julai 16, mwaka huu alikuwa ofisini kwake Kanda ya Dar es Salaam ambayo zamani ilikuwa Makao Makuu ya Wizara hiyo.Alidai kati ya saa saba hadi saa 10 jioni, walikuwa wanaangalia mfumo wa kielekroniki wanaoutumia kama unafanya kazi vizuri ambapo Kamishna Mkuu wa Ardhi, Mary Makondo aliwaita akiwaelekeza waende ofisi ya Waziri Lukuvi.

"Tulipoingia tulikuta baadhi ya watu ambao ni maofisa uchunguzi wa Takukuru, Waziri Lukuvi na Kiluwa. Tuliambiwa kuna bahasha ifunguliwe na sisi tuhakiki kilichomo.... ofisa uchunguzi alifungua na sisi kueka mezani mabunda manne yaliyofungwa," amedai Luge.Amedai baada ya kuzihakiki waliainisha fedha zote kwenye karatasi ya uchunguzi na kusaini na baada ya kukamilisha kazi hiyo waliruhusiwa kuondoka.

Akihojiwa na Wakili Madega kuhusu mahali walipozikuta fedha hizo, shahidi alidai kuwa walizikuta kwenye mfuko na kwamba ofisa uchunguzi ndiye aliyefungua na si Waziri Lukuvi wala mshitakiwa.Pia alidai hakushuhudia tendo lolote zaidi ya kuhakiki fedha isipokuwa alifanya kazi aliyoambiwa ya kuhakiki na hakujua fedha za nini.

Kwa upande wa Ofisa Uchunguzi wa Takukuru, Colman Lubisa (36) alidai kuwa hakushuhudia wakati Kiluwa akitoa rushwa kwa Waziri Lukuvi bali walipoingia ofisini walikuta fedha mezani ndipo walizihakiki."Kama Kiluwa asingefika kutokana na mwito wa Waziri Lukuvi kwa taratibu za Wizara ni lazima angeandikiwa barua ya mwito au notisi yoyote ile. Tulipata taarifa baada ya Waziri Lukuvi kupiga simu kwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Takukuru, Mbengwa Kasomambuto na kumueleza kuwa Kiluwa atafika ofisini akiwa na fedha Dola za Marekani 50,000," alidai Lubisa.

Pia alidai baada ya taarifa hiyo walikwenda kuandaa mtego ikiwemo kifaa cha kurekodia ili endapo mshitakiwa atafika na fedha hizo waweze kumkamata.Shahidi wa tano alidai baada ya kuandaa mtego walikaa nje kumsubiria mshitakiwa huyo na kati ya saa sita hadi saba alifika akiwa na begi.

"Mara baada ya kutoa fedha ambazo ni mabunda manne ya dola za Marekani yenye noti 100 kila moja na kuziweka mezani tuliingia na kumuweka chini ya ulinzi mshitakiwa na tuliita mashahidi wawili kuhakiki fedha zote," alidai Lubisa.Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Imani Madega, kuhusu kuchunguza mazingira ya rushwa kati ya Lukuvi na Kiluwa, alidai kuwa kitendo cha Waziri Lukuvi kumpa taarifa kwa njia ya simu mshitakiwa ni sahihi na endapo asingekwenda na fedha wasingejua kama anataka kutoa rushwa.

Alidai lengo la Kiluwa kutoa rushwa ni kumtaka Waziri alitelekeze alichokitaka katika hati 57 za kiwanja kilichopo maeneo ya Mlandizi na bila Waziri Lukuvi kutoa taarifa wasingejua mazingira hayo.Alidai tangu hati kusajiliwa ilikuwa na siku mbili pekee licha ya kutakiwa kutumika kwa uwekezaji baada ya miaka miwili huku umri wa hati ni miaka 66.

Pia alidai hakuwahi kupata malalamiko ya rushwa dhidi ya Kiluwa zaidi ya taarifa iliyotoka kwa Waziri Lukuvi na kwamba hawakutaka kuthibitisha uhalali wa taarifa hiyo kwa sababu aliyeitoa ni mtu wa serikali.Hata hivyo upande wa mashtaka umefunga kesi yao na Mahakama imeamua kuwa, mshtakiwa amekutwa na kesi ya kujibu, hivyo ataanza kujitetea Desemba 17 mwaka huu. 

Katika kesi hiyo Kiluwa anadaiwa kuwa Julai 16, mwaka huu, akiwa Mkurugenzi wa kampuni hizo mbili alitoa rushwa ya Dola za Marekani 40,000 ambazo ni sawa na Sh.milioni 90 kwa Waziri Lukuvi.Mshitakiwa anadaiwa kutoa fedha hizo ili asiwasilishe hati ya umiliki wa kiwanja namba 57 Block B Kikongo na D Disunyura kilichopo eneo la viwanda lililopo Kibaha mkoani Pwani. Kiluwa yupo nje kwa dhamana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post