Rais John Magufuli amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatakiwa kujitathmini kwanini watu wanakwepa kulipa kodi na kuamua kutumia wamachinga na wafanyabiashara wadogo kuwauzia bidhaa zao.
Ameyasema hayo leo Jumapili Desemba 2, 2018 wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa uboreshaji wa huduma za maji safi na maji taka katika kijiji cha Kimnyaki mkoani Arusha.
Amesema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa na tabia ya kutumia wamachinga kuuza bidhaa zao ili wasilipe kodi.
"Mnaweka viwango vikubwa ambavyo havilipiki jambo ambalo linafanya wafanyabiashara kukwepa, hivyo ni bora kuweka viwango vidogo vinavyolipika na wengi kuliko kiwango kikubwa kinacholipwa na watu wachache," amesema.
Amesema baadhi ya kodi zinazokusanywa na TRA ni za kuudhi kwani licha ya kuwa aliwaagiza kukusanya kodi kila sehemu ila sio za dhuluma.
Mbali na hilo aliwataka wamachinga kutumia vizuri fursa ya kufanya biashara kila sehemu waliyopewa ila sio katika kukwepa kodi.
"Serikali isiyokusanya mapato ni Serikali mfilisi, niwaombe sana wafichueni watu wenye tabia hiyo ili wasiwaharibie na muwe mnatoa elimu na sio kupeleka polisi kuwakamata wananchi wanaposhindwa kulipa kodi," amesema.