Rais John Magufuli ameahidi kutoa Sh700milioni kwa ajili ya kuboresha chuo cha taaluma ya Polisi kilichopo jijini Dar es Salaam kutokana na kukabiliwa na changamoto ya miundombinu ikiwamo uhaba wa majengo.
Akizungumza leo Ijumaa Desemba 21, 2018 katika sherehe za kufunga mafunzo ya maofisa wa polisi na wakaguzi wasaidizi wa jeshi hilo zilizofanyika viwanja vya chuo hicho, Rais Magufuli amesema atatoa fedha hizo ili kulinda heshima ya chuo hicho.
Amesema fedha hizo zitatolewa kabla ya Ijumaa wiki ijayo huku akisisitiza matumizi sahihi ya fedha hizo.
Awali Mkuu wa Chuo hicho, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Anthony Rutta akitoa taarifa ya mafunzo hayo alitaja changamoto ya uhaba wa miundombinu ikiwamo madarasa na mabweni na kuomba kiasi cha Sh700milioni.
“Nimekusikia umeomba Sh700milioni nitakuletea ili parekebishwe na kupendeza. Pamoja na kuwa sisi (Serikali) tunahamia Dodoma lakini hapa ni lazima papendeze,” amesema Magufuli.
Rais Magufuli ameagiza kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama zilivyopangwa na kusisitiza kuwa atafuatilia.
“Pale Jeshi la Magereza nilitoa fedha kwaajili ya kujenga nyumba za askari halafu hazikujengwa, sasa wakati mwingine unapata shida unatoa nyumba kwa ajili ya maaskari halafu hakuna nyumba, nimemuagiza kamishna wa magereza afuatilie hizo hela zimepotelea wapi,” amesema.
Social Plugin