Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA KUHUJUMU SHIRIKA LA NDEGE TANZANIA ATCL

Mawakala 10 wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ikiwamo kulisababishia Shirika hasara, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh. milioni 10.8.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ally Salum.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni, Fabian Ishengoma (34), Adam Kamara (27), Marlon Masubo (29), Neema Kisunda (24), Alexander Malongo (29) na Tunu Kiluvia (32).

Wengine ni Jobu Mkumbwa (30), Mohammed Issah (38), Godfrey Mgomela, Absalom Ambilikile na Janeth Lubega.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa kati ya Machi 10 na Oktoba 9, mwaka huu, mahali tofauti jijini Dar es Salaam na Mwanza washtakiwa kwa pamoja wakiwa mawakala wa ATCL, walilisababishia Shirika hilo hasara ya Sh.10,874,280.


Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa tarehe na mahali pa shtaka la kwanza, washtakiwa wote kwa pamoja walijipatia fedha hizo.

Shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa tarehe na mahali pa tukio la kwanza na la pili, washtakiwa wote walijipatia fedha hizo wakati wakijua ni mazalia ya udanganyifu yaliyotokana na utakatishaji fedha.

Hakimu alisema mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi na kwamba washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote hadi pale Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), atakapotoa kibali au upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya uhujumu uchumi na rushwa.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hakimu Salum alisema kesi hiyo itatajwa Januari 7, 2019, washtakiwa wamepelekwa mahabusu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com